Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Diwani Msemo akiwakaribisha wataalamu wa afya kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) waliofika ORCI kwa ajili ya kujifunza na kujionea huduma za matibabu ya saratani zinazotolewa katika Taasisi hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dkt. Diwani Msemo, akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa afya kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) pamoja na watumishi wa ORCI wakati wa ziara ya wataalamu kutoka MOI ya kujifunza na kujionea huduma za matibabu ya saratani zinazotolewa.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Mark Mseti akiwapa maelezo wataalamu kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) namna mashine ya Linear Accelerator (LINAC) inavyotumika katika kutoa tiba ya mionzi kwa kulenga seli za saratani kwa usahihi.

Daktari Bingwa wa Tiba ya Mionzi Nyuklia wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Bright Sangiwa akitoa maelezo kwa wataalamu kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kuhusu matumizi ya mashine ya PET/CT Scan (Positron Emission Tomography) ambayo inafanya kazi ya uchunguzi inayosaidia kuonyesha maeneo yenye mabadiliko ya kiutendaji mwilini na kusaidia wataalamu kutambua, kutathmini na kufuatilia saratani.
…………………
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imefanya ziara katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) kwa lengo la kujifunza na kuona kwa vitendo maendeleo ya miundombinu, teknolojia na huduma za kisasa zinazotolewa katika uchunguzi na matibabu ya saratani.
Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa yanayozitaka hospitali kubwa nchini kutembeleana, kubadilishana uzoefu na utaalamu pamoja na kujifunza mbinu mbalimbali za kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa kuwapokea wataalamu hao Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dkt. Diwani Msemo alisema ziara za namna hiyo ni muhimu kwa kuwa zinatoa fursa kwa taasisi za afya kufahamu uwezo, teknolojia na huduma zinazopatikana katika hospitali nyingine.
Alisema kutembeleana kwa hospitali kunawawezesha wataalamu kuona kwa vitendo hatua ambazo wenzao wamefikia katika uchunguzi na matibabu pamoja na kubaini maeneo ambayo wanaweza kushirikiana ili kuongeza ufanisi wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji wa Ubongo kutoka MOI, Dkt. Laurent Mchome alisema ziara hiyo imewapa fursa ya kujionea kwa karibu maboresho makubwa yaliyofanyika ORCI hususan katika miundombinu na vifaa tiba.
Alisema maboresho hayo yanaonyesha hatua kubwa iliyopigwa na ORCI katika kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma huku akibainisha kuwa baadhi ya mabadiliko hayo ni vigumu kuyatambua bila kufika na kujionea kwa macho.
Dkt. Mchome pia aliwahimiza wananchi kutopuuza dalili za magonjwa bali kufika hospitalini mapema wanapobaini mabadiliko yoyote yasiyo ya kawaida katika afya zao ili kupata uchunguzi na matibabu kwa wakati.
Akielezea ziara hiyo Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa ORCI, Dkt. Mark Mseti alisema wataalamu kutoka MOI walitembelea maeneo mbalimbali ya utoaji wa huduma ikiwemo kitengo cha tiba ya mionzi na kujionea mashine mpya za kisasa zenye uwezo mkubwa zinazotumika katika matibabu ya saratani.
Alisema pia ugeni huo ulipata fursa ya kutembelea mradi wa PET/CT Scan pamoja na kiwanda cha kuzalisha dawa za mionzi kupitia Cyclotron ambavyo ni miongoni mwa uwekezaji unaolenga kuongeza uwezo wa ORCI katika uchunguzi na matibabu ya saratani.
Katika ziara hiyo ORCI na MOI zimekubaliana kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya taasisi hizo ikiwemo kuimarisha vikao vya wataalamu vya kujadili wagonjwa wenye saratani za mifupa pamoja na saratani zinazohusisha ubongo na mishipa ya fahamu.
Ushirikiano huo unalenga kuongeza ushirikishwaji wa wataalamu kutoka pande zote mbili katika kufanya tathmini ya wagonjwa na kupanga huduma zinazofaa, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa matibabu na kuboresha huduma kwa wagonjwa.
Ziara hiyo inaendelea kuonyesha umuhimu wa hospitali na taasisi za afya nchini kujifunza kutoka kwa kila mmoja kubadilishana uzoefu na kutumia rasilimali na utaalamu uliopo kwa pamoja ili kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.
