Mkuu wa Utawala wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Kampasi ya Mwanza, Dkt. Laurent Sunda Joseph (kulia),  Mhadhiri Msaidizi na Mkuu wa Taaluma wa chuo hicho, Bahati Maneno, wakiwaonesha wananchi (hawapo pichani), jiko lnalotuma ol chafu lililobuniwa na wanafunzi

…………

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

CHUO cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Kampasi ya Mwanza, kimesema ubunifu wa bidhaa unaofanywa na wanafunzi wa chuo hicho kwa kutumia malighafi za ndani umevutia wananchi wanaotembelea banda la chuo hicho katika Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki (MEATF 2026).

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Utawala wa IFM, Kampasi ya Mwanza, Dkt. Laurent Joseph, wakati wa maonesho hayo yanayofanyika katika Uwanja wa Furahisha, Wilaya ya Ilemela, Mwanza, yakiwa na kauli mbui;. ‘ Usalama na Amani ni Kichocheo cha Biashara na Uwekezaji’.

 Dkt. Joseph alisema bidhaa hizo zimekuwa kivutio kutokana na ubunifu wa wanafunzi unaolenga kutumia malighafi zinazopatikana nchini katika kutengeneza bidhaa zinazoweza kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za jamii.

“Watu wengi wanaotembelea banda letu la IFM wanavutiwa na namna bidhaa zilizotengenezwa kwa malighafi za ndani, kutokana na ubunifu wa wanafunzi unaolenga kutatua changamoto za jamii,” alisema Mkuu huyo wa Utawala.

Alisema matumizi ya malighafi za ndani katika kutengeneza bidhaa yanaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa malighafi zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, huku yakitoa nafasi kwa ubunifu na uzalishaji wa bidhaa ndani ya nchi.

Dkt. Joseph pia alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuendelea kuboresha sekta ya elimu na kuwezesha taasisi za elimu ya juu kuandaa vijana wenye ujuzi unaoweza kuwawezesha kujiajiri na kushindana katika soko la ajira

“Chuo kimejipanga kuandaa vijana wabunifu watakaosaidia kukuza sekta ya viwanda na kutatua changamoto za jamii na ajira. Hivyo, tunampongeza Dkt. Samia na Serikali anayoiongoza katika utatuzi wa changamoto za jamii,” alisema.

Naye Mhadhiri Msaidizi na Mkuu wa Taaluma wa IFM, Kampasi ya Mwanza, Bahati Maneno, alisema ushiriki wa chuo hicho katika MEATF 2026 umefungua fursa ya taasisi hiyo kujitangaza kwa jamii na kuwafikia wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi.

Alisema licha ya kuwa ni mara ya kwanza kwa IFM kushiriki MEATF kama taasisi ya umma, maonesho hayo yamekuwa na manufaa kwa chuo hicho, ikiwamo kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma na shughuli zinazofanywa na IFM Kampasi ya Mwanza.

“Kila maonesho yanakuwa na wadau wake, ingawa kwetu IFM ni mara ya kwanza kushiriki maonesho ya MEATF 2026. Kama taasisi ya umma, bado kuna impact (matokeo chanya). Wananchi wamefumbua macho, wanauliza taarifa za taasisi yetu kwa hapa Mwanza,” alisema  Maneno.

Alisema maonesho hayo pia yamekuwa fursa kwa IFM kuwafikia watu wanaohitaji kujiunga na programu za elimu ya juu, hususan za Uzamili (Master’s) na Uzamivu (PhD), katika taaluma mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho.

“Maonesho hayo yametusaidia kibiashara, hasa katika kufanya tafiti na kutoa ushauri wa biashara namna zinavyofanyika, ikiwemo kupata wanafunzi wanaohitaji kujiunga na kozi za juu pamoja na aina ya huduma tunazotoa za ushauri kwa taasisi za umma,” alisema Mkuu huyo a Taaluma na Mhariri Msaidizi.

Maneno alisema IFM pia inafanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu, hivyo ushiriki wake katika maonesho hayo umeongeza fursa ya jamii na wadau mbalimbali kufahamu huduma hizo.

Alisema kupitia bidhaa za ubunifu na shughuli za ujasiriamali zinazooneshwa katika banda la IFM, chuo hicho kinapata fursa ya kuwasilisha uwezo wake katika tafiti, ubunifu na utoaji wa ushauri wa kitaalamu katika masuala ya biashara na maendeleo.