Na. Jeshi la Polisi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Paschal Katambi Patrobas, amezindua rasmi Kampeni ya Kitaifa ya Msamaha wa Usalimishaji wa Silaha Haramu kwa Hiari, akiwataka wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kutumia fursa hiyo kuzisalimisha ili kuimarisha amani na usalama nchini.
Uzinduzi huo umefanyika katika Uwanja wa Nyerere Square jijini Dodoma, Agosti 30 , 2026.
Waziri Katambi amesema kampeni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Tanzania katika kupambana na uzagaaji wa silaha haramu, ikiwa ni mwendelezo wa maamuzi ya Umoja wa Afrika ya kuunga mkono mpango wa kuondoa silaha haramu barani Afrika.
Amesema Serikali imetangaza msamaha wa kutoshitakiwa kwa mtu yeyote atakayesalimisha silaha anayoimiliki isivyo halali kuanzia Septemba 1 hadi Oktoba 31, 2026, ambapo usalimishaji utafanyika katika vituo vya Polisi, Ofisi za Serikali za Mitaa au kwa Watendaji wa Kata.
Aidha, Katambi amewataka wananchi wanaomiliki silaha kienyeji, silaha zilizorithiwa kutoka kwa ndugu waliofariki pamoja na wale wenye silaha kihalali lakini hawana tena uwezo au sababu ya kuendelea kuzitumia, kujitokeza kuzisalimisha.
Amesema kuendelea kumiliki silaha hizo kunaweza kuhatarisha usalama wa raia na mali zao, huku akisisitiza kuwa baada ya kipindi cha msamaha kumalizika, watakaobainika kumiliki silaha kinyume cha sheria watachukuliwa hatua.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Camillus M. Wambura, amesema msamaha wa usalimishaji wa silaha haramu kwa hiari ni hatua mahsusi ya Serikali inayolenga kuwapa wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria.
IGP Wambura alisema Jeshi hilo litaendelea na operesheni za kukabiliana na uhalifu, huku akisisitiza umuhimu wa kuzuia uhalifu kabla haujatokea kwa kupunguza idadi ya silaha haramu katika Jamii.

