Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imesimamisha shughuli za zaidi ya Bandari Kavu (ICD) sita jijini Dar es Salaam, hatua iliyolenga kuzipa nafasi za kujipanga upya na kuongeza uwezo wa kuhifadhi makontena pamoja na kuboresha usimamizi wa malori.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 31,2026 Jijini Dar es salaam kuhusu usimamizi na uendeshaji wa bandari kavu nchini, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Salum, alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kubaini changamoto katika matumizi ya maeneo ya ICD, ikiwemo malori kuachwa nje ya maeneo hayo na hivyo kuchangia msongamano katika maeneo yanayozunguka bandari.

Alisema ICD hizo zimeelekezwa kuandaa maeneo ya ndani kwa ajili ya kuhifadhi na kuhudumia malori, badala ya kuyaacha yakiwa yamezagaa katika maeneo ya nje, huku zikihitajika pia kuongeza uwezo wa kuhifadhi makontena ili ziweze kukabiliana na ongezeko la mizigo linalopitia Bandari ya Dar es Salaam.

Salum alisema hatua hiyo imekuja wakati Bandari ya Dar es Salaam ikiendelea kuongeza ufanisi na kuhudumia idadi kubwa ya makontena, hali ambayo imeongeza mahitaji ya maeneo ya kuyapokea baada ya kushushwa kutoka kwenye meli.

Alisema TASAC imeweka utaratibu unaozitaka ICD kutotumia zaidi ya asilimia 60 ya uwezo wake wa kuhifadhi makontena, ili kuhakikisha kunabaki nafasi ya kutosha kwa ajili ya shughuli za malori na shughuli nyingine za uendeshaji wa bandari kavu.

“ICD yenye uwezo wa kuhifadhi makontena 10,000 haipaswi kuzidi makontena 6,000 ili ndani ya ICD kuwe na nafasi ya shughuli za malori na shughuli nyingine za uendeshaji,” alisema Salum.

Alisema ongezeko la mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam limekuwa kubwa, ambapo kwa sasa bandari hiyo inapokea karibu makontena 4,000 kwa siku, hali inayohitaji bandari kavu kuongeza uwezo na kuimarisha mifumo yake ili kuzuia makontena kuzagaa ndani na nje ya maeneo ya bandari.

Salum alisema changamoto ya msongamano iliongezeka zaidi kuanzia Desemba hadi Machi, wakati uwezo wa baadhi ya bandari kavu uliopo haukuendana na idadi ya makontena yaliyokuwa yakifika, hali iliyosababisha msongamano kufika hadi ndani ya Bandari ya Dar es Salaam.

Alisema ongezeko la shehena ni fursa ya kiuchumi kwa Tanzania, lakini linahitaji maandalizi ya kutosha ya miundombinu na ushiriki wa sekta binafsi katika kuongeza maeneo ya kuhifadhi mizigo, kwa kuwa eneo la Bandari ya Dar es Salaam haliwezi kupanuliwa kwa urahisi kutokana na kuzungukwa na makazi na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus Abed, alisema ushirikishwaji wa sekta binafsi umeendelea kuongeza ufanisi wa bandari hiyo, huku kiwango cha mizigo kikiongezeka kutoka tani milioni 23.7 mwaka 2023 hadi tani milioni 33.7 katika mwaka wa fedha 2025/26.

Abed alisema ongezeko hilo la takribani tani milioni 10 ndani ya kipindi cha miaka miwili linaonesha kuongezeka kwa shughuli za biashara kupitia bandari hiyo, hali ambayo inahitaji uwekezaji zaidi katika ICD na miundombinu mingine ya kuhifadhi na kusafirisha mizigo ili kuendana na kasi ya ongezeko la shehena.