Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na Jamhuri ya Serbia, hususan katika maeneo ya biashara na uwekezaji, kilimo, utalii na Uchumi wa Buluu.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 31 Agosti 2026, jijini Belgrade, Serbia, alipokutana na Rais wa Jamhuri ya Serbia, Mhe. Aleksandar Vučić, katika Kasri la Serbia.

Amesema Tanzania na Serbia zina historia ndefu ya urafiki na ushirikiano uliojengwa katika misingi ya kuheshimiana, mshikamano na historia ya pamoja ndani ya Harakati za Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM), akibainisha kuwa urafiki uliokuwepo kati ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Rais Josip Broz Tito uliweka msingi muhimu wa mahusiano hayo.

Rais Dkt. Mwinyi pia amemfikishia Rais Vučić salamu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na ujumbe wa kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na Serbia.

Aidha, ameeleza kuwa Rais Dkt. Samia ameipongeza Serikali ya Serbia kwa kuandaa mkutano huo unaowakutanisha viongozi kutoka mataifa mbalimbali, huku akisisitiza kuwa uhusiano baina ya Tanzania na Serbia umeendelea kuimarika.

Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru Serikali ya Serbia kwa uamuzi wake wa kufungua Ubalozi wa kudumu nchini Tanzania, akieleza kuwa hatua hiyo ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

Amesema Serikali ya Tanzania tayari imetenga eneo katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Ubalozi wa Serbia pamoja na makaazi ya Balozi. Aidha, ameeleza kuwa nafasi ya Tanzania kama mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) inatoa fursa pana zaidi za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya Tanzania na Serbia katika ukanda huo.

Katika kuimarisha zaidi biashara na utalii, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza umuhimu wa kuwepo kwa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Serbia na Tanzania, zikihudumia Tanzania Bara na Zanzibar.

Naye, Rais wa Jamhuri ya Serbia, Mhe. Aleksandar Vučić, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza urafiki wa muda mrefu baina ya Serbia na Tanzania, akieleza utayari wa Serikali yake kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili.

Rais Vučić ameeleza kuwa Serikali ya Serbia imepokea mapendekezo mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili na kwamba inaendelea kuyafanyia kazi. Aidha, amesisitiza umuhimu wa Tanzania kuwa na Ubalozi wake kamili nchini Serbia, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili.

Vilevile, Rais Vučić ameunga mkono kuanzishwa kwa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Serbia na Tanzania, hatua itakayosaidia kuimarisha biashara, utalii na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Rais Dkt. Mwinyi yupo jijini Belgrade, Jamhuri ya Serbia, kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa Kumbukumbu ya Miaka 65 tangu kufanyika kwa Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi wa Harakati za Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM). Ziara yake pia inajumuisha mikutano na wafanyabiashara na wawekezaji wa Serbia, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha fursa za biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Serbia.