Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza mara baada ya kuapishwa kwa Mhe. Deogratius John Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliposhiriki hafla ya Uapisho huo Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma leo Agosti 29,2026.
………….
Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemtaka Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, kuitumikia nchi kwa utii, uaminifu, uzalendo, utu, busara, hekima na maarifa, huku akitanguliza maslahi ya Taifa.
Ametoa maelekezo hayo Agosti 29, 2026, katika hafla ya uapisho wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma.
Amesema nafasi hiyo ni dhamana aliyopewa na Watanzania, hivyo anapaswa kuitumia kwa kuwatumikia wananchi wote bila kujali tofauti zao na kuhakikisha majukumu anayokabidhiwa yanatekelezwa kwa maslahi ya Taifa.
Aidha ,amebainisha kuwa hakuna shule inayofundisha nafasi ya Makamu wa Rais, hivyo bidii, nidhamu, weledi na utayari wa kujifunza ni muhimu katika kumsaidia kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Pia ameongeza kuwa kujifunza kunahusisha kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali, pamoja na kujifunza kutoka kwa viongozi wengine anaofanya nao kazi.
Amesisitiza kuwa cheo cha Makamu wa Rais si ufalme bali ni dhamana, hivyo anayeshikilia nafasi hiyo anatakiwa kulitambua hilo na kuendelea kuitumikia Tanzania kwa uaminifu na uwajibikaji.
Aidha, amebainisha kuwa utekelezaji wa majukumu ya Serikali unahitaji umoja, mshikamano, ushirikiano, utulivu na uongozi bora ili kufikia matamanio na matarajio ya Watanzania.
Huku akibainisha ushirikiano na viongozi wengine ndani ya Serikali ni muhimu katika kuhakikisha majukumu yaliyopo yanatekelezwa na malengo ya maendeleo yanafikiwa kwa maslahi na usawa wa wananchi.

