Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma Joseph Kashushura,akizungumza kwenye kikao cha Boro ya nne cha Baraza la Madiwani.
…………….
Na Mwandishi Wetu,
Mbinga
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imetenga zaidi ya Sh milioni 358 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya kuboresha kilomita 45 za barabara, hatua inayolenga kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao kutoka maeneo ya uzalishaji hadi masokoni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Joseph Kashushura, amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha wakulima kusafirisha wenyewe mazao yao hadi masokoni na kupata bei nzuri, badala ya kulazimika kuwauzia walanguzi wanaofika mashambani na kununua kwa bei ndogo.
Kashushura ameyasema hayo wakati akieleza mikakati ya kuongeza tija ya uzalishaji katika kikao cha robo ya nne cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri uliopo Kigonsera wilayani Mbinga.
Amesema pamoja na uwepo wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA), Halmashauri imeamua kutumia mapato yake ya ndani kuchukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto ya barabara na hivyo kuharakisha maendeleo ya wakulima na uchumi wa Halmashauri.
Ametaja barabara zinazofanyiwa matengenezo kuwa ni Mkulumusi-Machimbo-Lukulasi, Amanimakolo-Kiwombi na Matiri-Lukiti, ambayo imefunguliwa kwa mara ya kwanza kwa lengo la kuunganisha vijiji hivyo na maeneo mengine ya Halmashauri.
Amesema barabara hizo ni muhimu kiuchumi kwa kuwa wananchi wa maeneo hayo ni wazalishaji na wasafirishaji wakubwa wa mahindi na kahawa, hivyo maboresho yake yatawawezesha kufikisha mazao yao sokoni kwa urahisi na kuongeza kipato.
Kashushura amemshukuru Meneja wa TARURA na timu yake kwa kusimamia kwa karibu matengenezo hayo, yanayofanyika kwa kiwango cha kawaida kwa kuchonga na kuweka vifusi katika maeneo hatarishi ili kuhakikisha barabara zinapitika.
Amesema mpango huo utaendelea kutekelezwa katika maeneo mengine ya Halmashauri hadi changamoto ya usafiri na usafirishaji itakapopungua kwa kiasi kikubwa, huku akieleza kuwa Halmashauri pia inaendelea kutekeleza miradi mingine ya maendeleo.
Ametoa mfano wa kutenga Sh milioni 100 kwa kila kata kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa shule mpya za sekondari katika kata za Ngima na Muongozi, huku Serikali Kuu ikitoa Sh milioni 560 kwa kila shule kwa ajili ya ujenzi.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Mbinga, Oscar Mussa, ameipongeza Halmashauri kwa kutenga fedha za mapato ya ndani kuboresha barabara, akisema Serikali pia imetenga Sh milioni 93 kwa ajili ya matengenezo yanayotekelezwa kwa kutumia nguvu kazi kupitia vikundi nane vilivyosajiliwa kwenye mfumo wa manunuzi.
Mwenyekiti wa Halmashauri, Desderius Haule, ameomba Serikali kupitia TARURA kuweka sheria maalum ya kuzuia magari yenye uzito mkubwa kupita kwenye barabara za vijijini ambazo haziruhusu magari yenye uzito unaozidi tani 20, huku Katibu wa CCM Wilaya ya Mbinga, Ali Simba, akiipongeza Halmashauri kwa kutekeleza Ilani ya CCM kupitia maboresho ya miundombinu ya barabara, afya na elimu.
