MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Modest Mkude akizungumza kwenye hafla hiyo.
…….
Na Happy Lazaro, Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Modestin Mkude, ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongeza juhudi katika kuboresha huduma kwa wafanyabiashara na walipa kodi, akisisitiza kuwa mazingira rafiki ya biashara ni muhimu katika kuongeza utii wa ulipaji kodi na kukuza uchumi.
Mkude ametoa kauli hiyo jijini Arusha alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, katika hafla maalum ya TRA ya kuwatambua walipa kodi na wadau waliotoa mchango katika shughuli za ukusanyaji wa mapato.
Amesema Serikali inatambua mchango wa wafanyabiashara katika uchumi na hivyo changamoto zinazoweza kuwakatisha tamaa kulipa kodi zinapaswa kushughulikiwa.
Amesema TRA inapaswa kuhakikisha huduma zinatolewa kwa wakati, wafanyabiashara wanapatiwa elimu ya kutosha kuhusu kodi na taratibu zinaeleweka ili kupunguza malalamiko na migongano isiyokuwa ya lazima.
“huduma bora kutoka kwa mamlaka ya kodi zinaweza kujenga uaminifu na kuwafanya wafanyabiashara kutekeleza wajibu wao kwa hiari.”amesema Mkude .
Aidha amewataka wafanyabiashara kutambua kuwa kulipa kodi ni wajibu wa kisheria na sehemu ya mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
Amewataka kuhakikisha wanasajili biashara zao, wanatoa na kudai risiti, wanatangaza taarifa sahihi za biashara na kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini vitendo vya ukwepaji kodi au magendo.
Mkude amesema mapato yanayokusanywa na Serikali kupitia kodi yana mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hivyo, amesema ushirikiano kati ya TRA na wafanyabiashara unapaswa kuimarishwa ili kuongeza mapato bila kuweka mazingira yanayoweza kuathiri shughuli halali za biashara.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Nguvila, ameitaka TRA kuendelea kuboresha mifumo na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato, akisema mafanikio ya Serikali katika kutekeleza mipango yake yanategemea uwezo wa kukusanya mapato ya ndani.
Dkt. Nguvila amesema Arusha ni miongoni mwa maeneo yenye shughuli kubwa za kiuchumi na hivyo Serikali, TRA pamoja na wafanyabiashara wanapaswa kuendelea kushirikiana kuhakikisha shughuli hizo zinachangia ipasavyo katika uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Ted Silkuwasha, amesema mafanikio ya ukusanyaji wa mapato mkoani Arusha yamechangiwa na ushirikiano uliopo kati ya Serikali, TRA na wafanyabiashara.
Amesema sekta za madini, kilimo, biashara na shughuli nyingine za uzalishaji zinaifanya Arusha kuwa eneo muhimu katika uchumi wa Tanzania.
Silkuwasha amewataka walipa kodi kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa hiari, huku TRA ikiendelea kusikiliza changamoto zao na kuboresha huduma.
Amesema mahusiano mazuri kati ya mamlaka ya kodi na wafanyabiashara ni msingi wa kujenga mfumo wa ulipaji kodi unaozingatia uwajibikaji na uzalendo.


