Na Mwandishi Wetu,
ARUSHA: Udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu, pamoja na uuzaji wa dawa zisizosajiliwa, umetajwa kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazokwamisha juhudi za udhibiti wa dawa na vifaa tiba katika Kanda ya Kaskazini.
Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Kaskazini, Proches Patrick akizungumza na Fullshangwe hivi karibuni amesema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakitumia vifungashio vya dawa zilizosajiliwa kughushi dawa, hali inayosababisha kuingia kwa dawa duni na bandia katika soko na kuhatarisha afya za wananchi.
Amesema changamoto nyingine ni uwepo wa dawa ambazo hazijasajiliwa zinazouzwa kwa siri na watu wasio waaminifu, akitolea mfano dawa ya VEGA 100, pamoja na uuzaji wa dawa za mifugo ambazo hazijasajiliwa na TMDA.
Kwa mujibu wa Meneja huyo, uwepo wa njia nyingi zisizo rasmi katika maeneo ya mipaka pia unachangia uingiaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi visivyofaa kwa matumizi au visivyoruhusiwa kuingia nchini.
Amesema TMDA Kanda ya Kaskazini imeendelea kuimarisha udhibiti kupitia ukaguzi wa bidhaa zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo katika mipaka na vituo vya forodha, pamoja na ukaguzi na ufuatiliaji wa ubora wa bidhaa zinazouzwa katika soko.
Ameeleza kuwa kazi nyingine zinazofanywa na ofisi za kanda ni pamoja na kusajili maeneo ya biashara zinazodhibitiwa na TMDA, yakiwemo maeneo ya waingizaji, watengenezaji na maduka ya vifaa tiba, pamoja na kutoa vibali vya kuingiza bidhaa nchini.
Katika kuimarisha udhibiti, TMDA pia imekuwa ikifanya uchunguzi wa awali wa sampuli za dawa kwa kutumia Maabara Hamishika (Min Lab Kit), hatua inayowezesha wataalamu kubaini kwa haraka ubora wa baadhi ya dawa zinazokutwa katika maeneo mbalimbali.
Takwimu za TMDA zinaonesha kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, jumla ya sampuli 754 zilifanyiwa uchunguzi wa awali kwa kutumia Maabara Hamishika, ikilinganishwa na sampuli 422 mwaka 2024/2025 na 401 mwaka 2023/2024.
Aidha, TMDA imeendelea kusimamia uondoaji wa bidhaa zisizofaa sokoni (Recall) na uteketezaji wa bidhaa ambazo hazikidhi viwango na hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026, jumla ya tani 8.85 za dawa zenye thamani ya takribani Sh milioni 682 zilikoteketezwa, ikiwa ni sehemu ya hatua za kulinda afya za wananchi.
