NA DENIS MLOWE , MBEYA
HALMASHAURI ya Manispaa ya Iringa imeibuka bingwa katika mchezo wa mpira wa wavu kwa wanaume katika Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Watumishi wa Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA) Kitaifa yaliyofanyika Jijini Mbeya mwaka 2026.
Manispaa ya Iringa ilitwaa ubingwa huo baada ya kuifunga timu ya Manispaa ya Dodoma Jiji kwa jumla ya seti 3-0 katika mchezo wa fainali, na hivyo kutwaa nafasi ya kwanza kati ya halmashauri 177 zilizoshiriki mashindano hayo.
Akizungumza mara baada ya timu yake kutwaa ubingwa huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, alisema mafanikio hayo yametokana na maandalizi mazuri yaliyowezeshwa na halmashauri pamoja na nidhamu ya wachezaji katika kipindi chote cha maandalizi.
Mlawa alisema halmashauri ilitenga bajeti kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo na kuhakikisha wanamichezo wanapata mahitaji muhimu, ikiwemo sare na vifaa vya michezo.
“Tulitenga bajeti kwa ajili ya SHIMISEMITA, lakini pia tumeweza kuwawezesha wanamichezo wetu. Tulianza kuwapa jezi, tracksuit na T-shirt zenye nembo ya Manispaa. Pia tuliwapa T-shirt nyingine kwa ajili ya kubadilisha wanapokuwa kwenye mapumziko,” alisema Mlawa.
Alisema pamoja na vifaa hivyo, siri kubwa ya mafanikio ilikuwa ni kuwapa wachezaji muda wa kutosha kufanya mazoezi, jambo lililosaidia kuimarisha uwezo wao kabla ya kuingia kwenye mashindano.
“Lakini kikubwa walikuwa kwenye mazoezi muda mrefu. Hiyo ndiyo siri kubwa; tuliwapa muda kwa ajili ya mazoezi,” alisema.
Ushindi huo unaifanya Manispaa ya Iringa kurejea kileleni baada ya kushindwa na wapinzani wao katika fainali ya mwaka uliopita, ambapo ilimaliza ikiwa mshindi wa pili huku timu iliyowafunga ikitwaa ubingwa.
Kwa upande wake, mafanikio ya mwaka huu yameonekana kuwa kisasi cha kimichezo kwa Iringa, baada ya timu hiyo kutumia uzoefu wa mwaka uliopita na maandalizi ya kutosha kuhakikisha inatwaa ubingwa.
Mashindano hayo yalifunguliwa na Profesa Riziki Shemdoe na kufungwa na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffary Haniu, katika Viwanja vya Sokoine Jijini Mbeya.
Ushindi wa Manispaa ya Iringa umeongeza heshima kwa halmashauri hiyo katika michezo ya watumishi wa Serikali za Mitaa, huku ukionyesha umuhimu wa uwekezaji katika michezo, maandalizi na kuwawezesha wanamichezo kupata mazingira bora ya kufanya mazoezi.