NA DENIS MLOWE IRINGA 

WANAFUNZI wa zamani (Alumni) wa Shule ya Sekondari Tosa Maganga wameungana kuchangisha Shilingi milioni 250 kwa ajili ya ununuzi wa basi la shule hiyo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo.

Akizungumza kuhusu mpango huo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Grayson Nyamoga, ambaye ni mmoja wa wanafunzi waliowahi kusoma katika Shule ya Sekondari Tosamaganga amesema Alumni wamekubaliana kushirikiana kuhakikisha shule hiyo inapata basi litakalosaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na shughuli mbalimbali za shule.

Nyamoga amesema mahitaji yaliyobainishwa na shule ni pamoja na ukarabati wa Bweni la Mandela, ukarabati wa Bweni la Mapinduzi, ununuzi wa samani kwa ajili ya ukumbi wa chakula (dining hall), pamoja na ununuzi wa basi ambalo linakadiriwa kugharimu Shilingi milioni 250.

Amesema Alumni wameamua kuanza na jukumu la kuchangia fedha za ununuzi wa basi hilo, wakiamini kuwa ni sehemu ya kurejesha kwa jamii na shule iliyowapa msingi wa elimu wanafunzi hao ambao sasa wako katika kada mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

“Tunawahamasisha wana Tosa na Alumni wote tushirikiane kuchangia fedha hizi, Shilingi milioni 250, ili tuweze kununua basi hilo na kuwakabidhi vijana wetu na wadogo zetu waliopo pale Shule ya Sekondari Tosa Maganga,” amesema Nyamoga.

Amesema basi hilo linatarajiwa kuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi na shule kwa ujumla, hasa katika kurahisisha usafiri wa wanafunzi wakati wa shughuli za kielimu, michezo, ziara za kitaaluma na shughuli nyingine zinazohitaji usafiri.

Nyamoga amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Alumni kuhakikisha maadhimisho ya miaka 100 ya Shule ya Sekondari Tosa Maganga yanaacha alama ya kudumu kwa kizazi cha sasa na kijacho, badala ya kuwa sherehe pekee.

Maadhimisho ya miaka 100 ya Shule ya Sekondari Tosamaganga yanatarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 8 hadi 10, 2026, ambapo Alumni wanatarajiwa kushiriki katika shughuli mbalimbali zitakazolenga kuimarisha uhusiano kati ya shule na wanafunzi wake wa zamani.

Amesisitiza kuwa mchango wa kila mwana Tosa ni muhimu katika kufanikisha lengo hilo, akiwataka Alumni kutumia fursa hiyo kuunga mkono maendeleo ya shule yao na kuhakikisha wanafunzi waliopo sasa wanapata mazingira bora ya kusoma na kufanya vizuri kitaaluma.

Amesema lengo la mwisho ni kuona juhudi hizo zinasaidia kuboresha mazingira ya shule na kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira rafiki yatakayowapa nafasi kubwa ya kufaulu na kutimiza ndoto zao.