šŸ“Dodoma

TUME ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imeanza ukaguzi wa taasisi, mashirika na wafanyabiashara wanaokusanya na kuchakata taarifa binafsi nchini, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha uzingatiaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44.

Hatua hiyo inalenga kubaini iwapo taarifa za watu zinakusanywa, kuchakatwa, kuhifadhiwa na kulindwa kwa kuzingatia matakwa ya sheria, huku taasisi zitakazobainika kukiuka masharti zikikabiliwa na hatua za kisheria, ikiwamo adhabu na faini.Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 28, 2026, na Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dk. Emmanuel Lameck Mkilia, ukaguzi huo utahusisha maeneo mbalimbali muhimu yanayohusu usimamizi wa taarifa binafsi.

Miongoni mwa mambo yatakayochunguzwa ni usajili wa taasisi zinazokusanya au kuchakata taarifa binafsi katika rejesta ya Tume, pamoja na usahihi wa taarifa zilizowasilishwa wakati wa usajili kwa mujibu wa Kifungu cha 14(1) na 14(2) cha sheria hiyo.

PDPC pia itakagua utekelezaji wa majukumu ya Afisa Ulinzi wa Taarifa katika taasisi husika, pamoja na taratibu zinazotumika katika ukusanyaji, uchakataji na uhifadhi wa taarifa binafsi.

Eneo jingine litakalopewa uzito ni usalama wa taarifa hizo, ambapo Tume itachunguza hatua zinazochukuliwa na taasisi kuzuia taarifa binafsi zisipotee, kuharibiwa, kubadilishwa au kuchakatwa bila idhini, kwa kuzingatia Kifungu cha 27(1) cha sheria.

Aidha, ukaguzi utahusisha namna taarifa binafsi zinavyosafirishwa au kuhamishwa nje ya nchi, huku PDPC ikisisitiza kuwa taratibu hizo zinapaswa kuzingatia masharti yaliyowekwa chini ya Vifungu vya 31 na 32 vya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Tume imewataka taasisi, mashirika na wafanyabiashara wanaokusanya au kuchakata taarifa binafsi kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kisheria, ikiwamo kupata ridhaa ya wahusika pale inapohitajika na kuhakikisha taarifa zinatumika kwa madhumuni halali na mahususi.

Wahusika pia wametakiwa kuzingatia haki za watu ambao taarifa zao zinakusanywa, kuwasilisha Ripoti ya Uzingatiaji kila robo ya mwaka na kuwa na Sera ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi iliyoidhinishwa na Tume.

PDPC imeonya kuwa taarifa binafsi hazipaswi kuhamishwa nje ya nchi kinyume na masharti ya sheria, huku taasisi zikihitajika kuweka mifumo madhubuti ya kuzuia matumizi au uchakataji usioidhinishwa wa taarifa hizo.

Baada ya hatua ya awali ya ukaguzi, Tume inapanga kutembelea taasisi, mashirika na wafanyabiashara mbalimbali nchini ili kufanya tathmini ya moja kwa moja kuhusu kiwango cha uzingatiaji wa sheria na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho.

PDPC imeeleza kuwa taasisi na wahusika watakaobainika kutokidhi matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi watachukuliwa hatua stahiki za kisheria, ikiwamo kutozwa adhabu na faini.