Wananchi wametakiwa kuthamini na kuendeleza utamaduni wao kwa kuwa ni msingi wa kuwaunganisha Watanzania, kuimarisha umoja na kujenga uzalendo kwa nchi yao.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Adam Malima, wakati akizindua Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni linalofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, Mkoani Morogoro.
Mheshimiwa Malima amesema tamasha hilo linawakutanisha Watanzania kutoka makabila mbalimbali, hivyo ni fursa muhimu ya kuendeleza umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa.
Amesema Watanzania wanapothamini na kuhifadhi tamaduni zao, wanachangia kujenga taifa lenye umoja na wananchi wenye uzalendo.
Katika tamasha hilo, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeshiriki kikamilifu kwa kutoa elimu kuhusu huduma za ardhi, huku wananchi wakipata fursa ya kupata huduma mbalimbali ikiwemo kupokea hati zao za umiliki wa ardhi.
Tamasha hilo linaendelea katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, likilenga kuenzi, kukuza na kuendeleza utamaduni wa Tanzania na linatarajiwa kuhitimishwa tarehe 29 Agosti 2026.