Amtaka mkandarasi kuongeza kasi na kukamilisha kabla ya AFCON 2027
Amshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kutoa fedha Bilioni 88 za ujenzi huo
………….
Na Mwandishi Maalumu  RS  Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege Lake Manyara wilaya ya Karatu, kutarahisisha usafiri kwa watalii wanaokwenda kwenye hifadhi na mbuga za wanyama pamoja na kupanua wigo wa idadi na ukubwa wa ndege kutua. 
Mhe. Makalla amesema hayo, alipotembelea na kikagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo, Agosti 27, 2026 na kubainisha kuwa, mradi huo  utawezesha kutua kwa ndege zenye uwezo wa kubeba hadi abiria 40, huku uwepo wa taa na lami ukiongeza usalama na uhakika wa kutua kwa ndege usiku.
“Faida za mradi huu ni pamoja na kuongeza idadi ya watalii na abiria, itaongeza pia aina na idadi ya ndege ikiwemo ndege zenye abiria kuanzia 40, zaidi uwepo wa taa utaongeza usalama wa abiria kutua kwa uhakika kwani taa na lami zitasaidia usalama.” Amesema CPA Makalla.
Aidha, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huo unaogharimu shilingi Bilioni 88 huku Mkandarasi akiwa amelipwa malipo ya awali Bilioni 12 na kumtaka Mkandarasi kuongeza kasi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kwa wakati kulingana na mkataba wa  Juni 2027 ili uwanja huo uanze kutumika kabla ya AFCON 2027.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania – TANROADS Mkoa wa Arusha, Mhandisi Regnald Massawe, amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia 9% na kumhakikishia mkuu wa Mkoa kusimamia vema na mradi huo utakamilika kwa wakati kulingana na mkataba kwa kuwa tayari ameshalipwa malipo ya awali.