Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilayani Tunduru(Tamcu Ltd)Marcelino Mrope akizungumza na wakulima wa Mbaazi wa Kijiji cha Namiungo.
…………….
Na Mwandishi wetu.
Tunduru
WAKULIMA wa zao la mbaazi wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wamejipatia zaidi ya Sh.bilioni 3.6 baada ya kuuza kilo 2,976,488 katika mnada wa kwanza uliofanyika katika Chama cha msingi cha ushirika Namiungo (Amcos) kata ya Namiungo.
Meneja Mkuu wa Chama kikuu cha Ushirika Tunduru(Tamcu Ltd)Marcelino Mrope amesema,mbaazi zote zimeuzwa kwa njia ya mnada kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani chini ya usimamizi wa soko la Bidhaa Tanzania(TMX) na bei wastani ilikuwa Sh.1,235 kwa kilo moja.
Akizungumza na wakulima wa kijiji cha Namiungo na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika Mrope alisema,Chama kikuu kupitia vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) katika msimu 2026/2027 kimeweka malengo ya kukusanya na kuuza kilo 20,700,000.
“Msimu uliopita 2025/2026 Tamcu kiliweka lango la kukusanya mbaazi kilo 15,000,000,lakini kilivuka lengo lililowekwa baada ya kufanikiwa kukusanya na kuuza kilo 17,490,006 na kufanya kuwa na ongezeko la uzalishaji kwa asilimia 14.24”alisema Mrope.
Alisema,mbaazi zilizokusanywa kutoka kwa wakulima,ziliuzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani na minada minane ilifanyika ambapo kilo 17,490,000 zenye thamani ya Sh. 12,462,737,164.00 ziliuzwa.
Alisema,ukusanyaji wa zao la mbaazi umeongezeka kutoka kilo 9,696,960 msimu 2024/2025 hadi kilo 17,490,006 msimu 2025/2026 ambayo ni sawa la ongezeko la asilimia 44.56 ambapo bei ilishuka 713 ikilinganisha na Sh.1,759.12 ya msimu 2024/2025.
Aidha alisema,kwa msimu wa mauzo 2026/2027 Chama kikuu tayari kimenunua viroba 425,700 kwa ajili ya kukusanya mbaazi vyenye uwezo wa kuhifadhi kilo 21,285,000 hivyo kutokana na makadirio ya uzalishaji wana ziada ya viroba vya kuhifadhi kilo 1,285,000.
Mrope alieleza kuwa,katika msimu wa mauzo 2025/2026 Chama kikuu kimepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kufanikisha usimamizi wa mauzo ya mbaazi kwa mfumo wa stakabadhi ghalani,kufanya malipo ya zaidi ya Sh.12,462,737,164.00 kwa wakulima na wadau wengine.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Sefu Dauda,amewataka watendaji wa vyama vya ushirika wilayani humo kuepuka kuchezea mizani kwa lengo la kuwaibia wakulima.
“Baadhi ya makarani sio waaminifu wamekuwa wakichezea mizani kwa kuwaibia wakulima,wote wanaohusika na michezo hii tuwaambie imetosha,mimi nina uhakika kwa hiki ninachozungumza kwani licha ya kuanza kutumia mizani ya Kidijitali,hata hivyo kuna baadhi ya makarani wetu wanajaribu kuchezea”alisema Dauda.
Dauda,amewaasa wakulima kuhakikisha akaunti zao za benki zinakuwa hai wakati wote badala ya kusubiri hadi msimu wa mauzo ya mazao unapofika.
Mkulima Ismail Mtamila,ameshukuru kupata bei nzuri katika mnada wa kwanza,hata hivyo ameiomba Serikali kuwasimamia wakulima ili waendelee kupata bei nzuri kwenye minada mingine.
Said Mpima,amewaomba wanunuzi kuongeza bei ya kununua mbaazi hadi kufikia 1,500 ili kuhamasisha wakulima waongeze uzalishaji katika msimu unaofuata kwa kuwa mbaazi kwa sasa ni zao mojawapo la biashara.
