Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe Albert Chalamila, amefanya ziara ya kutembelea na kukagua bandari kavu ya kilimanjaro iliyopo Kurasini Wilaya Temeke na kuwahakikishia wawekezaji wa ICD kuwa Serikali imejipanga kuunganisha bandari kavu zote na miundombinu ya reli huku akiitaka TARURA na TANROAD kuandaa mpango wa kujenga barabara za mzunguko katika maeneo ya bandari na bandari kavu, hatua inayolenga kupunguza msongamano wa malori katika Mkoa wa Dar es Salaam.
RC Chalamila ameyasema hayo agosti 27 mwaka 2026 wakati wa ziara ya kukagua shughuli za bandari na bandari kavu katika eneo la Kurasini ambapo alisisitiza umuhimu wa kuwa na maeneo ya kutosha ya maegesho ya malori yanayosubiri kupakia au kushusha mizigo ili kuepusha malori kusubiri kando ya barabara.
Aidha RC Chalamila ametumia nafasi hiyo kuitaka mamlaka ya mapato nchini TRA kuimarisha ukusanyaji wa mapato kupitia uwekezaji wa bandari kavu ambapo amewataka wawekezaji hao kujiepusha na ukwepaji wa kodi za serikali
Vilevile amesema ushirikiano kati ya TPA, Wizara ya Uchukuzi, TANROADS, TASAC na Taasisi nyingine za Serikali ni muhimu katika kuboresha mnyororo wa usafirishaji
Kwa upande wa, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus, amesema bandari hiyo inaendelea kuimarisha utendaji wake kwa kuongeza maeneo ya kuhifadhi na kuhudumia mizigo, ikiwemo eneo lenye ukubwa wa takribani mita za mraba 180,000 na kwamba wataendelea kushirikiana na bandari kavu ili kuongeza ufanisi
Naye Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Majini kutoka TASAC, Nelson Mlali, amesema mamlaka hiyo imeshasimamia na kurasimisha bandari takribani 29, zikiwemo bandari kavu, huku akieleza kuwa kuimarishwa kwa bandari hizo kutasaidia kupunguza msongamano wa malori kwenye barabara za Dar es Salaam huku Anitha Grewal Meneja wa Kilimanjaro ICD akieleza namna uwekezaji huo ulivyo ongeza ajira
Naye Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe Sixtus Mapunda, amesema uwepo wa Kilimanjaro ICD umeanza kusaidia kupunguza changamoto ya foleni za malori katika maeneo ya Kurasini na Temeke.

