NA DENIS MLOWE IRINGA
MEYA wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, amesema Serikali imefanikisha hatua kubwa ya kukamilisha ujenzi wa Machinjio ya Kisasa ya Ngelewala baada ya mitambo ya kisasa ya kuchinjia ng’ombe, mbuzi na kondoo kuwasili na kuanza kufungwa.
Ngwada amesema mitambo hiyo imenunuliwa kwa fedha zilizotolewa na Serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambapo Manispaa ya Iringa ilipokea Sh bilioni moja kwa ajili ya ununuzi wa mitambo hiyo.
Amesema kati ya fedha hizo, Sh milioni 920 zimetumika kuingia mkataba na kampuni ya Jipco kwa ajili ya ununuzi na ufungaji wa mitambo hiyo, huku akiwataka wananchi wa Iringa kutambua kuwa mradi huo ni halisi na unaendelea kutekelezwa.
“Mheshimiwa Rais katuletea pesa na tumefanya ununuzi wa vifaa ambavyo leo Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Iringa tumekuja kuvipokea rasmi,” amesema Ngwada.
Amesema awali Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika eneo hilo, ikiwemo jengo la utawala, maabara, jengo la kufulia, mfumo wa kuhifadhi na kudhibiti maji taka, uzio, zizi la kisasa pamoja na ukarabati wa awamu ya kwanza.
Ngwada, amesema Manispaa inatarajia kupokea tena Sh bilioni moja kwa ajili ya kukamilisha hatua ya mwisho ya mradi huo na kuhakikisha Machinjio ya Ngelewala yanafikia hadhi ya machinjio ya kisasa.
Amesema wazo la kujenga machinjio hiyo lilianza mwaka 2010, huku ujenzi ukianza baadaye na kuanza kutumika katika hali ya kawaida kabla ya kufanyika kwa ukarabati wa sasa.
Ngwada pia amekanusha taarifa kwamba baadhi ya vifaa vilivyowahi kuwekwa katika machinjio hayo vimepotea, akisema vifaa mbalimbali bado vipo na vingine vimeendelea kuwepo katika eneo hilo.
Amesema machinjio hayo yana cold rooms kwa ajili ya kuhifadhi nyama, ambazo awali hazikutumika kikamilifu kutokana na kiwango kidogo cha uchinjaji kilichokuwepo, lakini sasa zinatarajiwa kutumika zaidi baada ya kuongezeka kwa uwezo wa machinjio hayo.
Kwa upande wake, mtaalamu wa kufunga mitambo hiyo, Ali Kibada, amesema ana uzoefu wa kufunga mitambo ya machinjio katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Vingunguti, Songea na Kibaha.
Kibada amesema zoezi la ufungaji linatarajiwa kukamilika ndani ya wiki mbili, endapo hakutakuwa na changamoto, huku akieleza kuwa mitambo hiyo itaongeza ufanisi katika shughuli za uchinjaji.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa amesema kukamilika kwa Machinjio ya Ngelewala ni hatua muhimu kwa wananchi wa Manispaa ya Iringa ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakihitaji huduma ya machinjio ya kisasa.
Mlawa alisema baada ya Serikali kutoa fedha, manispaa ilianza mchakato wa kumpata mzabuni mwenye uwezo wa kukamilisha ukarabati na kufunga mitambo ya kisasa, huku wataalamu wakifanya ziara katika Manispaa za Songea na Kibaha pamoja na Geita kujifunza namna machinjio za kisasa zinavyoendeshwa.
Amesema kampuni ya Jipco ndiyo iliyopatikana kwa ajili ya kazi hiyo na tayari mitambo imewasili huku wataalamu wakiendelea na ufungaji.
Ameongeza kuwa Manispaa imeomba fedha kwa Serikali kwa ajili ya kununua jenereta ya kusubiri, ili kuhakikisha mitambo hiyo inaendelea kufanya kazi wakati wa kukatika kwa umeme.
Amesema wataalamu wanaofunga mitambo hiyo watabaki katika eneo la machinjio kwa muda kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa watumishi kuhusu uendeshaji na uchinjaji wa kisasa.
Aidha, amesema mitambo hiyo imepewa dhamana ya mwaka mmoja, hivyo endapo itapata hitilafu ndani ya kipindi hicho, mzabuni atawajibika kurekebisha changamoto hiyo kwa mujibu wa masharti ya mkataba.
Kwa sasa, wachinjaji waliokuwa wakifanya kazi katika Machinjio ya Ngelewala wamehamishiwa katika machinjio ya zamani ya Mlandege wakati ukarabati na ufungaji wa mitambo mipya ukiendelea.

