Awahimiza wazazi, walezi na wananchi kutoa ushirikiano wakati wote wa zoezi la utoaji chanjo
Awataka Wakuu wa Wilaya kuchukua hatua za kisheria kwa watakaokwamisha zoezi la chanjo
Na Mwandishi Maalumu RS  Arusha
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Alnason Nguvila, amewataka wazazi, walezi, walimu na wananchi kuhakikisha watoto wote wenye umri wa chini ya miaka 10, wanapata chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio, zoezi linalofanyika kuanzia tarehe 27 – 31 Agosti, 2026.
Akizungumza wakati akizundua rasmi zoezi la Chanjo Mkoa wa Arusha, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, kwenye Kituo cha Afya Levolosi Jijini Arusha, leo Agosti 27, 2026, Dkt. Nguvila amewataka viongozi wa dini na kimila kushirikiana na Serikali kuhamasisha jamii na kuokuwkana na imani potofu zinazoweza kuwafanya baadhi ya wazazi kuwaficha watoto wao.
Dkt. Nguvila amesema chanjo hiyo ni muhimu katika kuzuia watoto kupooza na na kupata ulemavu, kuokoa rasilimali watu na fedha kwa  kuhakikisha watoto wanakua wanakuwa na afya njema pamoja na kupunguza gharama na matumizi yasiyo ya lazima yanayotokana na matibabu ya magonjwa yanayoweza kuzuilika.
Aidha, Dkt.Nguvila amebainisha kuwa, chanjo hiyo inatolewa bure kwa watoto wote wa chini ya miaka 10, na kuwahimiza wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalamu watakaowafika kwenye maeneo yao kutoa chanjo huku akiwasisitiza Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha zoezi hilo linasimamiwa kikamilifu na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu watakaokwamisha zoezi au kupotosha jamii kuhusu chanjo.
“Kesho ya watoto wetu kiafya inajengwa leo. Mtoto ukimlea vyema na ukamkinga na magonjwa, anakuja kuwa nguvu kazi bora kesho,” amesema Dkt. Nguvila, akisisitiza kuwa Mkoa wa Arusha hautarajii kuwepo kwa vikwazo katika kuhakikisha kila mtoto anayestahili anapata chanjo hiyo.