NA FARIDA MANGUBE, MOROGORO

Mashindano ya Ngoma za Asili yameendelea kwa hamasa katika Tamasha la Nne la Utamaduni linalofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, mkoani Morogoro huku mikoa 10 ikifanikiwa kuingia katika hatua ya kumi bora.

Mikoa iliyofanikiwa kuingia katika hatua hiyo ni Mbeya, Mwanza, Morogoro, Pwani, Mtwara, Dodoma, Njombe, Arusha, Lindi na Dar es Salaam.

Mashindano hayo ni miongoni mwa matukio yanayovutia katika tamasha hilo yakilenga kuonyesha utajiri wa mila, desturi na sanaa za asili zinazopatikana katika jamii mbalimbali nchini Tanzania.

Washiriki kutoka mikoa hiyo wameonesha umahiri mkubwa kupitia ngoma zao za asili, wakitumia midundo, nyimbo, mavazi na miondoko ya jadi kuwasilisha historia na utamaduni wa jamii zao.

Akizungumza baada ya kufanikiwa kuingia katika hatua ya kumi bora, Mwajuna Omary mshiriki kutoka Mkoa wa Dar es Salaam, amesema juhudi, maandalizi na ushirikiano wa washiriki wa kikundi chake vimekuwa miongoni mwa sababu zilizowafikisha katika hatua hiyo.

Amesema kufuzu kwao ni matokeo ya kujituma katika mazoezi na kuhakikisha wanawasilisha ngoma zao kwa kuzingatia misingi ya utamaduni wao.

“Juhudi na maandalizi tuliyoyafanya yametufanya tufike katika hatua hii. Tumejipanga na tumekuwa tukifanya mazoezi kwa bidii ili kuhakikisha tunauwakilisha vizuri mkoa wetu na tamaduni zetu,” amesema Omary”.

Aidha, Omary amewataka Watanzania kutokukimbia au kuacha tamaduni zao, akisisitiza kuwa utamaduni ni sehemu muhimu ya utambulisho wa taifa na msingi wa mabadiliko katika jamii.

Amesema kizazi cha sasa kinapaswa kujifunza kutoka kwa wazee na kuiga baadhi ya mambo mema yaliyofanywa na vizazi vilivyotangulia, hususan katika kuhifadhi mila, desturi na mshikamano wa jamii.

“Ninawaomba Watanzania wasikimbie tamaduni zao, kwa sababu tamaduni ndiyo msingi wa mabadiliko. Tuige mambo mazuri ya enzi za wazee wetu na tuyahifadhi ili vizazi vijavyo viweze kujifunza kutoka kwetu,” amesema.

Kwa upande wake John Mwakatobe washiriki kutoka Mkoa wa Mbeya wameeleza kuwa kufika katika hatua ya kumi bora ni ishara ya kuongezeka kwa hamasa ya vijana katika kushiriki na kuendeleza sanaa za asili.