Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Bw. Charles Ngeleja Kadonya, amesema Bonde la Ziwa Victoria ni eneo la kimkakati lenye mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa na kuimarisha mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo miradi inayotekelezwa katika bonde hilo inapaswa kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
Bw. Kadonya amesema hayo akiwa mkoani Mwanza katika ziara ya kujifunza na kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali inayohusiana na Bonde la Ziwa Victoria, ambapo amesisitiza umuhimu wa kutumia fursa za biashara, uwekezaji, usafiri na rasilimali zilizopo katika ziwa hilo kuchochea maendeleo ya Kanda ya Ziwa na Taifa kwa ujumla.
Amesema utekelezaji wa miradi ya kikanda katika Kanda ya Ziwa una nafasi muhimu katika kuongeza ajira na kipato, kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya wananchi. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwawezesha wazawa kushiriki katika uwekezaji ili nao wawe sehemu ya mnyororo wa thamani na kunufaika na fursa zinazotokana na rasilimali za Ziwa Victoria.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya mkoa huo, amesema Serikali inaendelea na uwekezaji mkubwa katika miradi ya kimkakati, ikiwemo maboresho ya Uwanja wa Ndege wa Mwanza, miundombinu ya bandari na usafiri wa majini, hatua inayolenga kuongeza biashara, uwekezaji na kuimarisha muunganiko wa Mwanza na maeneo mengine ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika ziara hiyo, Bw. Kadonya ametembelea meli ya MV Mwanza – Hapa Kazi Tu, na kujionea huduma na miundombinu yake inayowezesha usafirishaji wa abiria na mizigo katika Ziwa Victoria, ikiwa ni sehemu ya uwekezaji unaolenga kuimarisha usafiri wa majini na biashara katika ukanda huo.
Pia ametembelea boti za uokozi katika Ziwa Victoria na kupata maelezo kuhusu mchango wake katika kuimarisha usalama wa usafiri wa majini na kukabiliana na dharura zinazoweza kujitokeza ziwani.
Vilevile, Katibu Mkuu ametembelea meli ya utafiti iliyofanyiwa ukarabati mkubwa kwa fedha za Serikali, inayotumika kufanya tafiti kuhusu samaki, ubora wa maji, hali ya ziwa na mifumo ya ikolojia ya majini, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za Ziwa Victoria.
Bw. Kadonya amesema ziara hiyo inalenga kujionea utekelezaji wa miradi inayohusiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki, kubaini changamoto na fursa zilizopo pamoja na kuona namna Tanzania inavyoweza kuongeza manufaa inayopata kupitia mtangamano wa kikanda.

