Na John Walter -Babati 
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Babati Vijijini, Mhe. Daniel Sillo, amezindua programu mbili mpya za shahada katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Kampasi ya Babati, akitaka chuo hicho kuendelea kubuni na kuanzisha kozi zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira na kusaidia kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana.
Programu hizo ni Shahada ya Sayansi ya Kompyuta (Bachelor of Computer Science) na Shahada ya Uhasibu katika Teknolojia ya Habari (Bachelor of Accounting in Information Technology), ambazo zimeelezwa kuwa na umuhimu katika kukabiliana na mahitaji ya uchumi wa kidigitali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Sillo amesema programu hizo ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa, hususan katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na wataalamu wenye ujuzi unaoendana na maendeleo ya teknolojia.
Amesema mifumo mbalimbali inayotumika katika sekta za umma na binafsi inahitaji wataalamu wenye ujuzi wa teknolojia, hivyo wahitimu wa programu hizo watakuwa na nafasi muhimu katika kusaidia serikali na jamii kutatua changamoto mbalimbali.
Sillo pia amewataka wanafunzi kutumia elimu wanayoipata kutambua changamoto zilizopo katika jamii na kubuni suluhisho badala ya kusubiri ajira, akisisitiza umuhimu wa elimu inayowawezesha vijana kuwa wabunifu na kujiajiri.
Kwa upande wake, Mkuu wa IAA Kampasi ya Babati, Dkt. Eliamani Sedoyeka**, amesema kuanzishwa kwa programu hizo kunaendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku akieleza kuwa chuo kinaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Dkt. Sedoyeka amesema Serikali imetoa Shilingi bilioni 3.7 kwa ajili ya ujenzi wa majengo mawili pamoja na uzio wa chuo, ambapo ujenzi unaendelea.
Ameongeza kuwa chuo kinatoa hosteli bure kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza, huku Kampasi ya Babati ikitoa jumla ya kozi 11 za Diploma.
IAA Babati ilianza kutoa huduma rasmi mwaka 2024, na sasa imeongeza programu hizo mbili za shahada katika hatua ya kupanua fursa za elimu ya juu kwa vijana wa Manyara na maeneo jirani.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati, Thobias Abwaro, amesema uwepo wa chuo hicho umesaidia kupunguza changamoto kwa wazazi ambao hapo awali walilazimika kuwapeleka watoto wao maeneo ya mbali kufuata elimu ya juu, jambo ambalo pia limekuwa likiongeza gharama.
Kwa upande wake, Mbunge wa Babati Mjini, Mhe. Emmanuel Khambay, amesema uwepo wa IAA Babati ni fursa kubwa kwa wakazi wa Babati na maeneo jirani ya Mkoa wa Manyara, kwani unawapa vijana fursa ya kupata elimu ya juu karibu na maeneo yao.
Kuongezeka kwa programu za teknolojia katika IAA Babati kunatajwa kuwa hatua muhimu katika kuandaa wataalamu watakaokidhi mahitaji ya uchumi wa kidigitali na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.