Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amewashukuru wadau mbalimbali walioshiriki na kuchangia kufanikisha Manyara Tanzanite Marathon 2026, akisema ushirikiano wao umewezesha kufanikisha mbio hizo za hisani zenye lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi na uwezeshaji wa wodi maalum ya kuwahudumia watoto njiti.
Sendiga ametoa shukrani hizo leo katika Mji wa Babati wakati wa Manyara Tanzanite Marathon 2026, zilizobeba kaulimbiu “Hatua Moja, Okoa Maisha ya Mtoto Njiti,” ambapo wananchi na wanariadha kutoka maeneo mbalimbali walishiriki kuunga mkono kampeni hiyo ya kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.
Amesema mafanikio ya mbio hizo yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, wadau wa afya, wafanyabiashara, taasisi mbalimbali na wananchi, ambao wameonyesha utayari wa kuchangia katika kuboresha huduma za afya kwa watoto njiti.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema lengo la Manyara Tanzanite Marathon 2026 ni kukusanya jumla ya shilingi bilioni 1.5, ambazo zitatumika katika ujenzi na uwezeshaji wa wodi maalum kwa ajili ya kutoa huduma kwa watoto njiti.
Amesema ushiriki mkubwa wa wadau katika mbio hizo umeonyesha kuwa jamii inaweza kushirikiana na Serikali kutatua changamoto mbalimbali za kijamii, hususan katika sekta ya afya.
Sendiga amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Manyara na washiriki kutoka mikoa mbalimbali kwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika mbio hizo, akisema hatua hiyo imeongeza hamasa na kuifanya kampeni hiyo kuwa ya pamoja.
Aidha, amewashukuru wanariadha walioshiriki katika mbio hizo, akisema ushiriki wao umeongeza mvuto wa tukio hilo na kuhamasisha jamii kuelewa umuhimu wa kuchangia huduma kwa watoto njiti.
Sendiga amesema Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha dhamira ya kuimarisha huduma za afya kwa watoto njiti inafikiwa, huku akisisitiza kuwa kila mchango, bila kujali ukubwa wake, una nafasi katika kuokoa maisha ya mtoto.
Amesema Manyara Tanzanite Marathon itaendelea kuwa jukwaa la kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuchangia masuala yenye manufaa kwa wananchi, hasa afya.
Amehitimisha kwa kuwashukuru tena wadau wote waliotoa mchango wao kwa njia mbalimbali, akisema mafanikio yaliyopatikana katika mbio hizo ni matokeo ya mshikamano na ushirikiano wao katika kuhakikisha watoto njiti wanapata huduma bora na nafasi kubwa ya kuishi.
Manyara Tanzanite Marathon 2026 imeongozwa na Mgeni Rasmi kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo, ambaye amepongeza uongozi wa Mkoa wa Manyara kwa ubunifu wa kuanzisha. mbio hizo.

