Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akivuta kifaa Maalum pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Dkt. Mostafa Kamal Madbouly kuashiria uzinduzi wa mitambo 9 ya kuzalisha umeme wa Megawati 2115 ndani ya Jengo la mitambo (Power House) katika Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP), Rufiji mkoani Pwani, tarehe 22 Agosti, 2026.
…………..
Na Fullshangwe, Rufiji
RUFIJI, PWANI: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kukamilika kwa Mradi wa Julius Nyerere wa kuzalisha umeme kumethibitisha uwezo wa Watanzania katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati, akisisitiza kuwa jambo kubwa zaidi kwa sasa ni kuendelea kuzilinda tunu za taifa za amani, utulivu, usalama na Umoja.
Akizungumza leo Agosti 22, 2026 wakati akizindua rasmi Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere kilichopo Rufiji mkoani Pwani, Rais Samia amesema mafanikio ya mradi huo ni alama ya umoja na utaifa, huku akiwapongeza viongozi, Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wakandarasi, wahandisi, wataalamu, mafundi, watumishi wa Serikali, sekta binafsi na wananchi wote walioshiriki katika utekelezaji wake.
Amesema kukamilika kwa mradi huo ni furaha kubwa kwa taifa kutokana na umuhimu wake katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na nishati ya kutosha na ya uhakika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo na ustawi wa wananchi. “Hakika ni furaha kubwa kwetu sote kushuhudia kukamilika kwa mradi huu ambao kwa miaka mingi umekuwa sehemu ya mipango na jitihada za taifa letu ili kuhakikisha tunakuwa na nishati ya kutosha na ya uhakika,” amesema.
Rais Samia amesema Desemba 22, 2022 alifika katika eneo hilo kushuhudia kufungwa kwa njia ya kuchepusha maji ya Mto Rufiji na kuanzishwa rasmi kwa ujazaji wa maji katika bwawa, ambapo ujazaji huo ulitarajiwa kuchukua takribani miaka mitatu, lakini kwa neema ya Mungu bwawa lilijaa ndani ya mwaka mmoja na nusu na kuanza majaribio ya uzalishaji umeme.
Amesema wakati wa ziara yake ya leo amezindua kituo cha kuzalisha umeme, ametembelea mitambo yake, tuta kuu pamoja na kituo cha kupokea na kusafirisha umeme kwenda kwenye gridi ya taifa na kujionea kuwa kila kitu kimekamilika na kinafanya kazi. “Tunatamka kwamba ndoto imetimia na mpango umewezekana,” amesema Rais Samia.
Kwa mujibu wa Rais Samia, kukamilika kwa mradi huo kunafundisha jambo muhimu katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati kwamba uamuzi wa kuanza mradi ni hatua moja, lakini mafanikio yake yanategemea nidhamu ya ufuatiliaji, uwezo wa kuhimili changamoto na kusimamia malengo yaliyowekwa.
Amesema historia ya mradi huo ni ndefu na inaanzia katika maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ya kutumia Mto Rufiji kuzalisha umeme wa uhakika na wa kutosheleza kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya nchi, akiwashukuru pia Marais waliomtangulia kwa kuendeleza na kuenzi maono hayo.
Rais Samia amemshukuru Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa ujasiri wa kuendeleza utekelezaji wa mradi huo mwaka 2019, licha ya changamoto zilizokuwapo, huku akiipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kusonga mbele na kusimamia kauli ya “kazi iendelee” hadi mradi ulipokamilika. Pia amewashukuru mawaziri na viongozi mbalimbali waliosimamia mradi huo katika hatua tofauti.
Amesema Tanzania haipaswi kukata tamaa inapofanya maamuzi yenye maslahi kwa taifa kwa sababu ya ugumu wa utekelezaji, bali inapaswa kuwa na uthubutu na uthabiti wa kusimamia maono na maamuzi hadi kufikia malengo yaliyowekwa. Amesema kwa kutambua mchango wa Marais wote waliotangulia, Serikali imetoa tuzo kwa viongozi hao kama sehemu ya kutambua mchango wao katika safari ya mradi huo.
Aidha, Rais Samia ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Kiarabu ya Misri kwa ushirikiano katika ujenzi wa mradi huo kupitia kampuni za Arab Contractors na Elsewedy Electric, akisema ushirikiano huo umeonesha namna nchi za Afrika zinapoungana zinaweza kutekeleza mambo makubwa kwa ustawi wa wananchi na bara zima. Pia amewapongeza wahandisi, mafundi, wataalamu na wafanyakazi wa Tanzania walioshirikiana na wakandarasi katika utekelezaji wa mradi.
Rais Samia amesema kituo hicho kinachangia sehemu kubwa ya umeme unaotumika nchini na ongezeko hilo limeongeza uwezo wa taifa kuzalisha umeme na kuwa na akiba ya kutosha, hatua inayotarajiwa kusaidia kupunguza changamoto za upatikanaji wa umeme na kuongeza fursa za biashara, uwekezaji, uzalishaji, ajira na kipato cha wananchi pamoja na pato la taifa.
Amesema Serikali inaendelea kuimarisha gridi ya taifa ili umeme unaozalishwa katika kituo hicho uweze kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali nchini, akitaja ujenzi wa njia ya umeme ya kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma pamoja na upanuzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Zuzu mkoani Dodoma. Amewataka Waziri wa Nishati na TANESCO kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa haraka.
Amesema Serikali imeendelea kupanua upatikanaji wa umeme nchini, huku akiwapongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na washirika wa maendeleo kama African Development Bank na World Bank kwa mchango wao katika kusambaza umeme vijijini. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutafuta na kuzalisha umeme kupitia vyanzo vingine ikiwemo jua, upepo na vyanzo vingine ili kukidhi mahitaji yatakayoongezeka kutokana na uwekezaji na shughuli za kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amewataka Watanzania kutunza mazingira na vyanzo vya maji vinavyolisha Bwawa la Julius Nyerere ili mradi huo uweze kudumu kwa miaka mingi, huku akizitaka taasisi za Serikali kuratibu na kusimamia kwa karibu uhifadhi wa mazingira katika maeneo yanayohusiana na mradi. Pia amewataka viongozi kuchukua tahadhari kutokana na utabiri wa mvua kubwa na kuhakikisha miundombinu inalindwa dhidi ya uharibifu.
Akihitimisha hotuba yake, Rais Samia amesema mradi huo umethibitisha uwezo wa Tanzania na unapaswa kuwa kichocheo cha utekelezaji wa miradi mingine ya kimkakati, lakini akasisitiza kuwa mafanikio hayo hayawezi kuwa na maana bila amani, utulivu, usalama na umoja wa kitaifa. “Amani, utulivu na usalama wa taifa letu si wajibu wa vyombo vya ulinzi na usalama pekee, bali ni wajibu wetu sote. Tuendelee kuzilinda tunu hizi kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo na ustawi wa taifa letu,” amesema.

