Na Fullshangwe, Rufiji
RUFJI, PWANI: Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema kukamilika na kuzinduliwa kwa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) ni matokeo ya juhudi mahususi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha mradi huo unakamilika na kuongeza uwezo wa Taifa wa kuzalisha umeme.
Akizungumza mbele ya Rais Samia katika hafla ya uzinduzi wa JNHPP wilayani Rufiji, mkoani Pwani, leo Agosti 22, 2026, Ndejembi amesema kituo hicho kina mitambo tisa, ambapo kila mtambo una uwezo wa kuzalisha megawati 235, hivyo kuwa na uwezo wa jumla wa kuzalisha megawati 2,115.
Amesema uzalishaji huo umeongeza uwezo wa Tanzania kukidhi mahitaji ya umeme yanayotokana na shughuli za kiuchumi na uwekezaji, huku ikiifanya nchi kuwa daraja muhimu la kuunganisha masoko ya nishati ya umeme barani Afrika kupitia East African Power Pool na Southern African Power Pool.
Ndejembi amesema uwezo wa Taifa wa kuzalisha umeme umefikia megawati 4,646 dhidi ya mahitaji ya juu ya Gridi ya Taifa ya megawati 2,175, hivyo Tanzania kuwa na ziada ya umeme inayoweza kutumika kufanya biashara na nchi jirani.
Amesema Serikali tayari imeingia makubaliano na Zambia kwa ajili ya kuiuzia umeme, huku ikiwa na makubaliano na Kenya kuhusu biashara ya umeme kulingana na mahitaji ya kila nchi, na ikiendelea na mazungumzo na nchi nyingine jirani.
Waziri huyo amesema JNHPP si kituo cha kuzalisha umeme pekee, bali ni sehemu ya mfumo mzima wa miundombinu inayowezesha umeme kuzalishwa, kusafirishwa, kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa na kuwafikia watumiaji kwa uhakika.
Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya usafirishaji wa umeme, ikiwemo kukamilika kwa njia ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, ambayo imewezesha umeme unaozalishwa JNHPP kufika Dodoma kwa uhakika.
Ndejembi amesema baada ya laini ya Chalinze-Dodoma kuanza kufanya kazi, kiwango cha juu cha matumizi ya umeme nchini kimeongezeka kutoka megawati 2,130 hadi megawati 2,280 ndani ya siku tatu, huku Serikali ikiendelea na ujenzi wa laini ya Chalinze-Mkuranga-Kinyerezi kwa lengo la kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme.
Amesema Serikali pia inaendelea na ujenzi wa laini ya msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa zaidi ya kilomita 617 kutoka Iringa kupitia Mbeya na Songwe hadi Rukwa, ambayo imefikia takribani asilimia 98 ya ujenzi wake.
Amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa laini ya Songea-Tunduru-Masasi kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara, huku ikiwekeza pia katika kituo cha kupokea umeme cha Ibadakuli mkoani Shinyanga.
Ndejembi amesema Serikali iko katika maandalizi ya kuanza ujenzi wa Tanzania-Uganda Interconnector, ambao utasaidia kusafirisha umeme hadi maeneo ya uzalishaji wa madini katika mikoa ya Geita na Kanda ya Ziwa, ili kukidhi mahitaji ya wachimbaji.
Amesema pamoja na kuongeza uzalishaji, Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya usambazaji ili kupunguza changamoto za kukatika kwa umeme zinazotokana na uchakavu wa nguzo, laini na transfoma katika baadhi ya maeneo.
Amesema kukamilika kwa JNHPP kunaiwezesha Tanzania kuangalia mbele zaidi kutokana na mahitaji ya umeme kuendelea kukua sambamba na uchumi, viwanda, biashara, madini, kilimo cha kisasa, usafirishaji na huduma za kijamii, huku Serikali ikilenga kufikisha uzalishaji wa umeme hadi megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 kwa kutumia vyanzo mbalimbali.

