Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya Kigeri Estates Ltd ,Paul Lyimo akizungumza katika mahafali hayo jijini Arusha .Mkuu wa shule hiyo ,Sr.Beatrice Macha akizungumza kwenye mahafali.hayo.jijini Arusha

Wahitimu wa darasa la saba wakitumbuiza kwenye mahafali hayo jijini Arusha leo

 Happy Lazaro,Arusha .

Arusha .WAZAZI wametakiwa kushirikiana kwa karibu na walimu katika malezi na ufuatiliaji wa maendeleo ya watoto wao, kwani jukumu la kumlea mtoto haliwezi kuachwa mikononi mwa mwalimu pekee bali linahitaji ushirikiano wa pande zote mbili.

Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na mgenirasmi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya Kigeri Estates Ltd ,Paul Lyimo katika mahafali ya 4 ya darasa la saba na mahafali ya 6 ya elimu ya awali(PP2) katika shule ya mchepuo wa kiingereza ya Sun of Hope iliyopo Usa river wilayani Arumeru mkoani Arusha .

 Amesema mtoto anapopelekwa shuleni, mzazi hapaswi kuacha majukumu yake, bali anapaswa kuendelea kumfuatilia mtoto anapokuwa nyumbani, kujua kama anafanya kazi za shule, kusoma, kuuliza maswali na kumpa msaada pale anapohitaji.

Lyimo amesema ushirikiano huo haupaswi kuchukuliwa kama njia ya kulaumiana kati ya wazazi na walimu, bali ni namna ya kukumbushana na kuimarishana katika kuhakikisha watoto wanapata malezi na elimu bora.

 Amefafanua kuwa, wazazi wanapaswa kuwa karibu na watoto wao badala ya kuwaacha muda mwingi wakitumia simu au kutazama televisheni bila uangalizi, akisisitiza kuwa malezi bora yanahitaji muda, upendo, ufuatiliaji na ushirikiano wa pande zote.

Aidha, amewataka wazazi kuwa wazi na uongozi wa shule kuhusu changamoto zinazohusiana na ulipaji wa ada, akisema hata pale mzazi anapochelewa kupata fedha, ni muhimu kuwasiliana na shule na kutoa taarifa ya lini anatarajia kukamilisha malipo. 

“utaratibu huo utaiwezesha shule kupanga vizuri shughuli zake na kuhakikisha huduma za elimu zinaendelea bila changamoto kubwa.”amesema .

Hivyo, amewataka wazazi kutowasiliana na shule pale tu wanapokuwa na tatizo, bali kujenga utamaduni wa mawasiliano ya mara kwa mara na uongozi ili changamoto zinapojitokeza ziweze kutafutiwa ufumbuzi kwa pamoja.

Aidha Lyimo ameipongeza shule kwa kazi kubwa inayofanywa na walimu katika kuwaandaa wanafunzi kitaaluma na katika malezi.

 Amesema ameshuhudia matokeo ya juhudi za walimu, wakiwemo masista na walimu wengine, katika kuwajenga wanafunzi siyo tu katika masomo ya kawaida, bali pia katika lugha kama Kiingereza na Kifaransa pamoja na maeneo mbalimbali yanayowasaidia wanafunzi kujiandaa kwa maisha yao ya baadaye.

Aidha amewataka wahitimu kuendelea kuwa na bidii, nidhamu na kutokata tamaa katika safari yao ya elimu na maisha. 

“kila mwanafunzi ana kipaji na njia yake ya kufikia mafanikio, kwani baadhi watajikita katika biashara, wengine sayansi na taaluma nyingine, hivyo wanapaswa kutumia fursa walizonazo kujenga maisha yao na kuwafanya wazazi wao wajivunie.”amesema Lyimo.

Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo ,Sr.Beatrice Macha amesema kuwa ,tangu kwa kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 2020 imepata mafanikio makubwa kielimu ikiwemo upatikanaji wa vitabu vya kujifunzia ,kuimarisha malezi na maadili ya wanafunzi,kuboresha mazingira ya shule,pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu .

Sr.Macha amesema kuwa,katika kuendelea kuboresha taaluma shule imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuendelea kusimamia nidhamu ya wanafunzi ili waweze kutumia muda wao vizuri katika kujifunza,kuimarisha ushirikiano kati ya shule na wazazi katika kufuatilia maendeleo ya watoto,kuboresha mbinu za ufundishaji ili kila mwanafunzi aweze kuelewa na kufikia uwezo wake .

“Shule bado ina mahitaji ya maboresho ya miundombinu ikiwemo ujenzi wa uzio wa kudumu wa shule (ukuta),maboresho ya uwanja wa michezo ,kuongeza magari ya shule pamoja na kuongeza vifaa vya uchapishaji kutokana na ongezeko la shughuli za kitaaluma na kiutawala .”amesema Sr Macha.

Aidha pamoja na mafanikio hayo ametaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na baadhi ya wazazi kuchelewa kulipa ada kwa wakati,ushiriki hafifu wa baadhi ya wazazi katika kufuatilia maendeleo ya watoto wao na usimamizi wa kazi za nyumbani .

Aidha amewataka wanafunzi hao kuendelea kuwa na bidii katika masomo ,kuwa na nidhamu ,kuheshimu wazazi walimu na watu wote wanaokutana nao kwani elimu ni ufunguo wa maisha na mafanikio yao ya baadaye huku akiwaasa changamoto wanazokutana nazo isiwe sababu ya kukata tamaa bali ziwe nafasi ya kujifunza na kuwa bora zaidi 

Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa shule hiyo ,Sr .Innocensia Mbuya amewataka wanafunzi hao wakawe mabalozi wema popote watakapokuwa wa kutangaza shule yao huku wakitanguliza mbele maadili yote waliyofundishwa wakiwa shuleni hapo.