Harambee ya kuchangisha fedha na vifaa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Jimbo la Kilimanjaro, kupitia Usharika wa Msitu wa Tembo, Mtaa wa Israel, imefanyika kwa mafanikio huku viongozi na wadau mbalimbali wakijitokeza kuunga mkono ujenzi huo.
Katika harambee hiyo, Mdau wa maendeleo wilayani Simanjiro, Taiko Ole Kulunju, ameendelea kuonesha mshikamano wake katika kusaidia shughuli za maendeleo kwa kuchangia kiasi cha shilingi milioni 4 pamoja na mifuko 100 ya saruji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha ujenzi wa jengo hilo unakamilika.
Taiko Ole Kulunju amesema mchango wake ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za waumini na uongozi wa kanisa katika kuhakikisha wanapata jengo lenye mazingira bora kwa ajili ya ibada pamoja na shughuli mbalimbali za kijamii.
Amesisitiza kuwa maendeleo hayawezi kufikiwa na mtu mmoja pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa viongozi, taasisi za dini, wafanyabiashara, wadau wa maendeleo na wananchi kwa ujumla, bila kujali tofauti zao.
Harambee hiyo pia imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, akiwemo Frank Ole Leshwa, mwakilishi wa Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Mhe. James Ole Milya, pamoja na madiwani mbalimbali kutoka Wilaya ya Simanjiro. Kwa pamoja, viongozi hao wamechangia zaidi ya shilingi milioni 21, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za waumini katika kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo.
Kwa upande wake, Diwani mwenyeji na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Mh Kaleya Mollel, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo, amewashukuru viongozi, waumini na wadau wote waliojitokeza kuchangia ujenzi huo kwa fedha, vifaa na namna nyingine mbalimbali.
MH . Kaleya amesema ushirikiano na moyo wa kujitolea uliooneshwa na washiriki wa harambee hiyo ni mfano mzuri wa mshikamano unaopaswa kuendelezwa katika jamii, hususan katika kusaidia miradi yenye manufaa kwa wananchi.
Lengo la harambee hiyo ni kuchangisha fedha na vifaa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo la kanisa, ikiwemo kukamilisha hatua mbalimbali za ujenzi kutoka kwenye lenta ya kwanza na ya pili hadi hatua ya upauaji, pamoja na mahitaji mengine muhimu.
Mchango wa Taiko Ole Kulunju na viongozi wengine katika harambee hii unaonesha kuwa maendeleo ya jamii hayapaswi kubaki kuwa jukumu la taasisi au kundi moja pekee.
Pale viongozi, taasisi za dini, wafanyabiashara na wananchi wanapoweka tofauti zao pembeni na kuungana kwa lengo moja, miradi ya kijamii hupata nguvu na kasi ya kukamilika.
Harambee hii ni mfano unaothibitisha kuwa mshikamano, kujitolea na uwajibikaji wa pamoja vinaweza kuwa chachu ya maendeleo endelevu katika jamii.

