Dar es Salaam: Kundi la kusaidiana na wadau wa Madale Group limeungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki katika ibada ya kumuaga marehemu Mzee Robinson Nchiyiki Yimba, kabla ya mwili wake kuanza safari kuelekea mkoani Kigoma kwa ajili ya mazishi.
Ibada hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya taratibu za kumuaga marehemu, ambaye alifariki dunia tarehe 15 Agosti 2026, akiwa amefikisha umri wa miaka 89.
Akizungumza katika ibada hiyo, mmoja wa viongozi wa Madale Group ameeleza kuwa kundi hilo limeguswa na msiba huo na kuona umuhimu wa kusimama pamoja na familia katika kipindi hiki cha majonzi.
Amesema ushiriki wao katika ibada hiyo ni ishara ya upendo, mshikamano na faraja kwa familia ya marehemu, huku akitoa pole kwa watoto, wajukuu, vitukuu, ndugu na jamaa wote walioguswa na msiba huo.
Kwa mujibu wa wasifu wa marehemu uliotolewa na familia, Mzee Robinson Nchiyiki Yimba alizaliwa tarehe 1 Julai 1937 katika kijiji cha Mkabogo, mkoani Kigoma.
Marehemu alijishughulisha na biashara kati ya mikoa ya Mwanza na Dodoma na pia aliwahi kuwa kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Mkoa wa Kigoma, akihudumu kama Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kigoma Vijijini kuanzia mwaka 1990 hadi 2005.
Katika maisha yake ya familia, marehemu alijaaliwa kupata watoto 25, wajukuu 138 na vitukuu 72.
Familia imeeleza kuwa pamoja na huzuni ya kumpoteza mpendwa wao, inafarijika kwa maisha aliyoyaishi, upendo alioutoa kwa familia na jamii pamoja na kizazi kikubwa alichokiacha.
Baada ya ibada hiyo ya kumuaga, mwili wa marehemu Mzee Robinson Nchiyiki Yimba umeanza safari kuelekea mkoani Kigoma, ambako taratibu za mazishi zitaendelea.
Madale Group imeendelea kutoa pole kwa familia na kuwaomba ndugu, jamaa na marafiki kuendelea kuwa pamoja katika kipindi hiki cha majonzi.
BWANA ametoa, BWANA ametwaa; jina la BWANA lihimidiwe.



