Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii katika maeneo ya kimkakati ikiwemo biashara na uwekezaji, kilimo, madini, nishati, usafirishaji, miundombinu, afya na teknolojia ya kidijitali.
Makubaliano hayo yamefikiwa tarehe 18 Agosti 2026, kufuatia mazungumzo kati ya Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa DRC, Mhe. Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo, yaliyofanyika katika Ikulu Ndogo Zanzibar.
Katika biashara na uwekezaji, Rais Samia amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na DRC kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na wawekezaji, kurahisisha biashara ya mipakani na kuongeza uzalishaji wa bidhaa zenye thamani. Nchi hizo pia zimekubaliana kuimarisha huduma za forodha na miundombinu ya mipakani.
Katika sekta ya madini, Tanzania na DRC zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika utafiti wa kijiolojia, uchimbaji, uchakataji na kuongeza thamani ya rasilimali hizo ndani ya Afrika, sambamba na kuendeleza ujuzi na matumizi ya teknolojia.
Kwa upande wa usafirishaji na nishati, viongozi hao wamekubaliana kuongeza matumizi ya bandari na korido za usafirishaji ili kuwezesha biashara , pamoja na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya reli, barabara, bandari na nishati.
Aidha, Tanzania na DRC zimesisitiza umuhimu wa amani na usalama kuwa msingi wa maendeleo, huku Rais Tshisekedi akieleza kuwa ziara hiyo imeweka msingi wa kuimarisha ushirikiano na kusisitiza umuhimu wa Afrika kuongeza thamani ya rasilimali zake ndani ya bara ili kukuza ajira na kuhakikisha utajiri wa Afrika unanufaisha Waafrika.

