
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof. Prof. Appolinary Kamuhabwa, akizungumza na waandishi wa leo Agosti 17, 2026 jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa kitengo maalumu cha matibabu ya meno kwa watoto wanaohitaji dawa za usingizi au ganzi, sambamba na kusainiwa kwa hati ya makubaliano (MoU) kati ya MUHAS, Chuo Kikuu cha Ankara pamoja na Shirika la Ushirikiano na Uratibu la Türkiye (TİKA)

…………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimeimarisha ushirikiano na Chuo Kikuu cha Ankara pamoja na Shirika la Ushirikiano na Uratibu la Türkiye (TİKA), kwa lengo la kuendeleza huduma za afya za kibingwa, mafunzo, utafiti na ubunifu nchini Tanzania.
Akizungumza leo Agosti 17, 2026 jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa kitengo maalumu cha matibabu ya meno kwa watoto wanaohitaji dawa za usingizi au ganzi, sambamba na kusainiwa kwa hati ya makubaliano (MoU) kati ya taasisi hizo.
Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa, amesema kitengo hicho, kilichoanzishwa katika Shule ya Meno ya MUHAS, kimeanza kutoa huduma kwa watoto wenye matatizo ya kinywa na meno ambao hawawezi kufanyiwa matibabu wakiwa macho, ambapo tangu huduma hiyo ilipoanza mwezi Mei mwaka huu, watoto 27 tayari wamepatiwa matibabu.
Prof. Kamuhabwa amesema kuanzishwa kwa kliniki hiyo ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya ushirikiano huo, kwani inatoa huduma maalumu kwa watoto wanaohitaji matibabu ya meno kwa kutumia dawa za usingizi au ganzi, huduma ambayo haikuwahi kupatikana nchini Tanzania.
Ameeleza kuwa huduma hiyo ni muhimu kwa watoto wanaoogopa sindano, wasioweza kuvumilia matibabu ya meno wakiwa macho au wenye changamoto za kiafya zinazofanya matibabu ya kawaida kuwa magumu.
Mbali na huduma za meno, ushirikiano huo umejikita pia katika tiba za dharura, ambapo MUHAS imepokea gari la wagonjwa litakalotumika kutoa huduma na kuwafundisha wanafunzi kuhusu namna ya kukabiliana na hali za dharura.
Prof. Kamuhabwa amesema “Mpango huu utaimarisha uwezo wa Tanzania katika kukabiliana na dharura, hususan usimamizi wa ajali, kuhakikisha njia ya hewa ya mgonjwa inabaki wazi na kumstabilisha kabla ya kufikishwa hospitalini”
Kuhusu hati ya makubaliano iliyosainiwa, amesema haijaweka kiwango maalumu cha fedha, bali imeweka msingi wa taasisi hizo kuandaa na kutekeleza miradi ya pamoja na kutafuta fedha kutoka TİKA na washirika wengine wa maendeleo.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ankara, Prof. Dr Necdet Ünüvar, amesema kuanzishwa kwa kitengo hicho na ushirikiano katika tiba za dharura ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano kati ya taasisi hizo.
Ameongeza kuwa matibabu ya meno kwa watoto kwa kutumia dawa za usingizi ni eneo muhimu na lenye changamoto, hivyo uwepo wa huduma hiyo ni hatua kubwa kwa Tanzania.
Mkuu wa Shule ya Meno ya MUHAS, Prof. Ferdinand Machibya, amesema ushirikiano huo utasaidia katika utafiti wa pamoja, mafunzo ya uzamili, kubadilishana wanafunzi na wataalamu, matumizi ya akili bandia katika uchanganuzi wa picha za kitabibu, ujenzi wa uwezo wa huduma za tiba na uandaaji wa maombi ya pamoja ya ruzuku.
Prof. Machibya amesema mafanikio ya ushirikiano huo hayapaswi kupimwa kwa idadi ya makubaliano yaliyosainiwa pekee, bali kwa kuangalia matokeo katika utafiti wa pamoja, mafunzo ya wanafunzi na wasomi, ubunifu, machapisho, upatikanaji wa ruzuku na maboresho ya huduma za afya katika jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TİKA nchini Tanzania, Halim Ömer, amesema shirika hilo limetekeleza zaidi ya miradi 350 ya ushirikiano nchini Tanzania katika sekta mbalimbali, zikiwemo elimu, kilimo, mifugo, afya, mafunzo ya ufundi, maji na usafi wa mazingira.
Amesema kuwa TİKA imewezesha kitengo cha meno kwa kutoa vifaa vya ganzi, vifaa vya meno, vifaa vya kusaidia njia ya hewa kwa watoto, vifaa vya kupumulia na vifaa vya huduma za dharura.
Ömer amesema mpango wa kuanzisha shule ya wahudumu wa huduma za dharura utajengwa juu ya mafunzo ya kukabiliana na majanga na dharura yaliyotolewa mwaka 2024, ambapo zaidi ya madaktari 50 wa huduma za dharura walipatiwa mafunzo.
