Mkurugenzi wa Ereto Pre and Primary School, Ebenezer Kilepo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mahafali yao jijini Arusha leo.
Mwalimu Mkuu wa Ereto Pre and Primary School, Isaiah Mwakio akizungumza na waandishi wa habari katika mahafali hayo jijini Arusha.
Wahitimu wa darasa la saba katika shule ya mchepuo wa kiingireza ya Ereto pre and primary wakitumbuiza katika mahafali hayo.
………..
Na Happy Lazaro, Arusha .
Wazazi na walezi wametakiwa kutenga dakika tano hadi kumi kila siku kwa ajili ya kuzungumza na watoto wao, wakielezwa kuwa mawasiliano ya karibu kati ya mzazi na mtoto ni msingi muhimu wa kujenga familia bora na jamii yenye maadili.
Wito huo umetolewa jijini Arusha na Mkurugenzi wa Ereto Pre and Primary School, Ebenezer Kilepo, wakati akizungumza katika mahafali ya pili ya Darasa la Saba yaliyofanyika shuleni hapo, ambapo jumla ya wanafunzi 29 wamehitimu.
Kilepo amesema wazazi hawapaswi kusubiri matatizo yatokee ndipo waanze kuzungumza na watoto, bali wanapaswa kutenga muda wa kukaa nao, kuwasikiliza, kujua mahitaji yao pamoja na changamoto wanazokutana nazo katika maisha ya kila siku. Amesisitiza kuwa watoto wanapaswa kujengwa kwa upendo badala ya kutumia muda mwingi kuwakemea.
“Dakika chache za mazungumzo zinaweza kusaidia mzazi kuelewa kinachoendelea katika maisha ya mtoto na kuchukua hatua mapema,” amesema Kilepo.
Amefafanua kuwa mzazi anapotenga hata dakika tano hadi kumi kila siku kukaa na mwanawe, kumsikiliza na kuzungumza naye, hujenga uhusiano wa karibu unaomfanya mtoto kuwa huru kumweleza changamoto anazokutana nazo. 
Kwa mujibu wa Kilepo, mtoto anayejisikia kupendwa na kusikilizwa huwa na uwezekano mkubwa wa kumshirikisha mzazi wake pale anapokabiliwa na tatizo.
Akirejea kauli ya profesa mmoja, Kilepo amesema, “Ni bora kuwasha mshumaa kuliko kulaani giza,” akieleza kuwa wazazi wanapaswa kuchukua hatua kwa kuzungumza na watoto badala ya kukaa kimya na kuanza kulalamika baada ya matatizo kujitokeza.
Amesema familia zitakapoanza kujenga utamaduni wa kuzungumza, kusikilizana na kusaidiana, zinaweza kufanya mambo makubwa katika maisha ya watoto, familia na jamii kwa ujumla. 
Ameongeza kuwa mawasiliano mazuri ni sehemu muhimu ya kujenga kizazi chenye mwelekeo, maadili na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha.
“Unapotenga dakika tano mpaka kumi na kuongea na mwanao, unamjenga kiupendo. Akishakuwa na upendo, hata anapopata tatizo atakuambia, hata anapokuwa na changamoto atakuambia,” amesema Kilepo.
Kilepo amesema moja ya changamoto zinazowakabili baadhi ya wazazi ni pilikapilika za maisha na majukumu ya kazi, ambazo huwafanya washindwe kupata muda wa kutosha wa kuzungumza na watoto wao. 
Hata hivyo, amesisitiza kuwa kila mzazi anapaswa kutafuta muda, hata kama ni mfupi, kwa ajili ya mazungumzo na mtoto.
“Maisha yamebadilika sana. Sisi tulipokuwa wadogo tulikuwa na changamoto zetu, lakini sasa hivi changamoto za watoto wetu zinahusisha zaidi sayansi na teknolojia,” amesema.
Aidha, amewataka wazazi kutokuwa walezi wa mahitaji ya kimwili pekee, bali wawe wasikilizaji na walezi wa karibu wa watoto wao ili waweze kuelewa mapema changamoto zinazowakabili na kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi katika kipindi ambacho teknolojia na mazingira ya kijamii yanabadilika kwa kasi.
Kilepo amesema Ereto Pre and Primary School imeendelea kuweka mkazo katika malezi yenye maadili, akieleza kuwa kuporomoka kwa maadili katika jamii ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji ushirikiano wa shule na wazazi. 
Amesema shule hiyo imejikita katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu inayoambatana na malezi bora na maadili mema yatakayowawezesha kuwa watu wenye mchango chanya katika jamii. “Tunajitahidi kuweka maadili katika hali nzuri,” amesema.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Ereto Pre and Primary School, Isaiah Mwakio, amewataka wanafunzi waliomaliza Darasa la Saba kuendelea kuwa makini wanapokuwa nyumbani na kuzingatia sheria, taratibu na maadili waliyofundishwa shuleni, akisisitiza kuwa nidhamu ni msingi muhimu wa mafanikio katika masomo na maisha kwa ujumla.
Mwakio amesema wanafunzi hao wanapaswa kutumia likizo na muda wa kuwa nyumbani kwa namna inayowajenga, huku wakiepuka tabia na mienendo inayoweza kuwa kikwazo katika safari yao ya elimu. 
Ameongeza kuwa elimu waliyopata shuleni inapaswa kuonekana kupitia tabia, heshima na uwajibikaji wao wanapokuwa nje ya mazingira ya shule.
“Wazazi tunawaomba sana muendelee kuwa karibu na watoto, kuwafuatilia na kuwashauri katika hatua mbalimbali za maisha, kwani ni muhimu kuwabana watoto ili wasijiingize katika makundi yasiyofaa,” amesema Mwakio.
Mwakio amewashukuru wazazi wa Ereto Primary kwa kujitokeza kwa wingi na kushirikiana na shule katika kufanikisha mahafali hayo, akisema ushirikiano kati ya wazazi, walimu na wadau wa elimu umeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya shule hiyo.
Mwakio ameongeza kuwa,mahafali hayo ni ya pili kufanyika shuleni hapo, baada ya mahafali ya kwanza yaliyofanyika mwaka uliopita ambapo wanafunzi walifanya vizuri na kufikia wastani wa Daraja A. 
Kwa mwaka huu, amesema shule inatarajia kupata matokeo makubwa zaidi kutokana na juhudi zinazofanywa na walimu, wanafunzi na wazazi, huku akieleza kuwa wanaendelea kumtegemea Mungu katika matokeo hayo.
Mwakio amewataka wahitimu hao kujiamini, kuepuka vishawishi na kufanya kila wawezalo ili kufikia ndoto zao. Pia amewahakikishia kuwa shule itaendelea kuwathamini na kuwaombea mafanikio katika kila hatua ya maisha yao.