Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo akizungumza kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo Profesa Adolf Mkenda.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Profesa Said Mohamed akizungumza kwenye mkutano huo jijini Arusha.

………..
Na Happy Lazaro, Arusha
WATAALAMU wa tathmini ya elimu kutoka Afrika na mataifa mengine wamekutana jijini Arusha kujadili namna ya kutumia teknolojia ya Akili Mnemba (AI) katika kuboresha mifumo ya upimaji na tathmini ya elimu, huku Tanzania ikieleza utayari wa kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia.
Mkutano huo wa 42 wa Mwaka wa Shirikisho la Vyama vya Tathmini ya Elimu Afrika (AEAA) unaofanyika kuanzia Agosti 17 hadi 21, 2026, umewaleta pamoja washiriki kutoka nchi 28 za Afrika na nje ya bara hilo ambapo majadiliano yake yanalenga kuangalia fursa na changamoto zinazotokana na matumizi ya AI katika sekta ya elimu, hususan katika mitihani na tathmini.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Profesa Said Mohamed, amesema Tanzania inatambua kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia na imejiandaa kutumia fursa zinazotokana na AI katika kuimarisha mifumo ya utahini na tathmini nchini.
Profesa Said amesema teknolojia imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku katika karne ya 21, hivyo sekta ya elimu haiwezi kujitenga na maendeleo hayo.
Ameeleza kuwa AI inaendelea kuleta mabadiliko katika maeneo mbalimbali na kwamba matumizi yake katika elimu yanaweza kusaidia kuboresha namna tathmini zinavyofanyika.
Mbali na masuala ya teknolojia, Profesa Said amewataka wajumbe wa mkutano huo kutumia muda wao wakiwa Arusha kujenga mahusiano, kubadilishana uzoefu na kutengeneza kumbukumbu nzuri.
Amesema thamani ya maisha haipaswi kupimwa kwa mali pekee, bali pia kwa uzoefu ambao mtu anaupata na mahusiano anayojenga.
Ameeleza kuwa tafiti za saikolojia zimeonyesha kuwa watu wanaowekeza zaidi katika uzoefu na kujenga kumbukumbu wanaweza kupata furaha kubwa kuliko wale wanaotumia nguvu kubwa katika kumiliki vitu.
“Mtu anayechagua kununua uzoefu au kujenga kumbukumbu anaaminika kuwa mwenye furaha zaidi kuliko anayechagua kununua vitu vya mali,” amesema Prof .Said.
Akizungumzia hali ya afya barani Afrika, Profesa Said amesema changamoto mbalimbali za kiafya katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara bado zinaendelea kuchangia ongezeko la vifo na kufanya umri wa kuishi katika eneo hilo kuwa chini ya wastani wa dunia.
Mkutano huo umebebwa na kaulimbiu “Rethinking Educational Assessment in Africa in the Age of AI”, inayosisitiza umuhimu wa kuangalia upya mifumo ya tathmini ya elimu ili iweze kuendana na mabadiliko yanayoletwa na Akili Mnemba.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Carolyne Nombo, amesema matumizi ya AI yanapaswa kuwa nyenzo ya kuongeza ubora na ufanisi wa tathmini, huku maamuzi ya kitaalamu yakiendelea kufanywa na wataalamu wa elimu.
Profesa Nombo amesema pamoja na fursa zinazotokana na AI, matumizi yake yanapaswa kuambatana na uwajibikaji, uadilifu na kuzingatia nafasi ya utaalamu wa binadamu katika mifumo ya elimu.
Naye Rais wa Chama cha Tathmini ya Elimu Afrika (AEAA), Dkt. Ashetu Kebede Gichoro, amezitaka nchi za Afrika kuchukua hatua za haraka katika kuingiza teknolojia kwenye mifumo ya tathmini, akisema kuchelewa kunaweza kulifanya bara hilo kutegemea mifumo iliyotengenezwa nje ya Afrika.
Amesema AI inaweza kusaidia kubadilisha namna mitihani na tathmini zinavyofanyika, ikiwemo kutengeneza mitihani inayoweza kuendana na uwezo wa mwanafunzi, kuchambua takwimu na kusaidia katika uundaji wa njia binafsi za ujifunzaji.
Hata hivyo, amesema matumizi ya AI yanahitaji kuzingatia masuala ya usawa, maadili na usalama wa data. Kwa mujibu wake, Afrika inapaswa kujenga mifumo yake ya kiteknolojia ambayo ni huru, salama na inayozingatia mahitaji ya bara hilo.
“Kama Afrika haitajenga mfumo wake huru wa tathmini uliojumuisha teknolojia, tunahatarisha kuwa watumiaji wa mifumo iliyoagizwa kutoka nje ambayo haiakisi uhalisia wetu wala kutumikia matarajio,” amesema.
Dkt. Gichoro pia amesema matumizi hafifu ya takwimu za tathmini katika kutengeneza sera na kupanga maendeleo ni miongoni mwa changamoto zinazopaswa kushughulikiwa.
Ameongeza kuwa ukosefu wa miundombinu ya kutosha ya kidijitali, changamoto katika ubora wa data na kutounganishwa kwa mifumo ya takwimu na sera ni vikwazo vinavyohitaji ufumbuzi.
Amesisitiza kuwa kutokana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani, Afrika inapaswa kuchukua hatua sasa katika kuunganisha teknolojia na mifumo ya tathmini ya elimu ili kuhakikisha maendeleo ya elimu yanaendana na mahitaji ya kizazi cha sasa na kijacho.
