AMINA Juma Masenza amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA) Mkoa wa Mwanza, kwa kura 25 katika uchaguzi wa viongozi wa jumuiya hiyo, na kupewa dhamana ya kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano.
Mkutano Mkuu huo wa uchaguzi wa JUWAKITA uliofanyika leo, na kusimamiwa na Naibu Katibu Mkuu (Dini) wa BAKWATA Makao Makuu, Mohamed Khamis Said, akisaidiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Chanila, ambaye ni Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Mwanza, kwa niaba ya Sheikh Nuhu Mruma.
Hadija Liganga Mfaume alichaguliwa kuwa mjumbe wa Mkutano Mkuu wa JUWAKITA Taifa baada ya kupata kura 24, akifuatiwa na Sikitu Abubakar aliyepata kura 23 na Fatuma Abdallah Bajber aliyepata kura 21.
Kwa upande wa wajumbe wa Kamati Kuu ya Mkoa, Aisha Said Marzuku, Asha Omar, Asha Juma, Asma Ali Said na Hajat Safina Shaaban walipata kura 25 kila mmoja na kuchaguliwa katika nafasi hizo.
Wajumbe wengine katika Kamati Kuu hiyo ya Mkoa ni Mwanaidi Hamis aliyepata kura 24, Husna Mganda na Hamida Mwinyikambi waliopata kura 23 kila mmoja, Rahma Juma aliyepata kura 22 na Sharbano Abubakar aliyepata kura 20.
Akizungumza baada ya kutangaza matokeo, Msimamizi wa uchaguzi Mohamed Khamis Said alisema washindi wote wanastahili kupewa hati za ushindi, akisisitiza hata ambao kura zao hazikutosha kushinda nafasi walizowania ni sehemu ya JUWAKITA Mwanza na wanapaswa kuendelea kushirikiana.
Alisema viongozi hao wanapaswa kukaa pamoja na kuchakata mambo mbalimbali yatakayosaidia kuleta maendeleo kwa wanawake na jamii kwa ujumla, huku akiwataka kuweka mbele umoja na ushirikiano katika kipindi cha uongozi wao.
Naye Sheikh Hassan Kabeke aliwataka wanawake waliochaguliwa kutambua kuwa wamepewa dhamana ya kuwatumikia wenzao, huku wale ambao kura zao hazikutosha akiwataka wasikate tamaa wala kuwa na kinyongo kutokana na matokeo ya uchaguzi.
Pia, aliwataka wanawake kuwa waangalifu katika matumizi ya maneno na kuepuka kauli zinazoweza kuwaumiza au kuwagawa wenzao, akisisitiza kulinda utu na mshikamano ndani ya jumuiya.
“Akina mama tuchunge ndimi zetu tusiseme maneno ya kuwachoma watu, maana utu wa mwanadamu uko ndani ya pango lake yaani kinywani mwake,” alisema Sheikh Kabeke na kuwataka wajumbe wa JUWAKITA kurejea katika shughuli zao wakiwa wamoja, akisisitiza kuwa BAKWATA ni taasisi inayowaunganisha na kuwapa nafasi ya kushirikiana katika kusimamia masuala ya dini na jamii.
Sheikh Kabeke aliwataka viongozi wapya kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wanawake, akitaja mikopo yenye masharti magumu na rushwa ya ngono, hivyo watafakari namna ya kuwavusha wanawake kiuchumi na kusaidia kukabiliana na mmomonyoko wa maadili kwa watoto na jamii.
Kwa upande wake, Masenza, aliwashukuru wajumbe kwa kumwamini kuiongoza jumuiya hiyo kwa kura 25, akisema anathamini dhamana waliyopewa viongozi hao na kuomba Mungu awape busara na hekima katika kuwatumikia wanawake wa Kiislamu.
Alisema waliochaguliwa wamepewa dhamana ya kuwahudumia wanawake, hivyo viongozi wenzake washirikiane na kuhakikisha JUWAKITA inakuwa chombo cha kuwainua wanawake na kusaidia jamii.
“Waliotuchagua wametupa dhamana ili tuwahudumie akina mama. Mungu atupe busara na hekima katika kuwatumikia na kuongoza wanawake wa Kiislamu,” alisema Masenza.

