Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.Timu ya Jiji la Arusha imeagwa rasmi kuelekea mkoani Mbeya kushiriki Michuano ya Shirikisho la Michezo na Sanaa za Watumishi wa Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA), huku viongozi wakiiweka timu hiyo katika mazingira ya matumaini makubwa ya kufanya vizuri na kurejea na vikombe.
Akizungumza wakati wa kuwaaga wanamichezo hao, viongozi wa Serikali ya Jiji la Arusha wamewataka washiriki kutumia vyema maandalizi waliyofanya na kushiriki kwa nguvu katika michezo yote 15 watakayoshindana.
Imeelezwa kuwa tofauti na miaka ya nyuma ambapo Jiji la Arusha lilikuwa likipeleka idadi ndogo ya watumishi kushiriki michezo michache, mwaka huu limeongeza ushiriki kwa kupeleka watumishi wengi watakaoshiriki katika michezo yote 15.
Viongozi hao pia wamewakumbusha wanamichezo hao umuhimu wa kuzingatia nidhamu, umoja na ushirikiano, wakisisitiza kuwa wanakwenda Mbeya kuiwakilisha Serikali ya Jiji la Arusha na wanapaswa kulinda heshima ya taasisi hiyo.
“Tunawaamini na tunatarajia mtarejea na makombe. Msiende kushiriki tu, nendeni mkashindane na kushinda,” ulisisitiza uongozi wakati wa kuwaaga wanamichezo hao.
Kwa upande wake, Afisa Habari na Mstahiki wa Timu ya Watumishi wa Jiji la Arusha, Mwalimu Emmanuel Reziki Joel, maarufu kama Iman Mzungu, amesema timu hiyo iko tayari kwa mashindano na imejipanga kuhakikisha inapata matokeo chanya.
Amesema wanamichezo hao wana ari na nguvu kubwa ya ushindani, huku wakiahidi kupambana katika kila mchezo ili kurejea Arusha wakiwa na mafanikio.
Naye mwalimu na mwanamichezo Djeni Twarira, kutoka Serikali ya Kata ya Sinoni, ameishukuru Serikali ya Jiji la Arusha kwa msaada na maandalizi yaliyowezesha idadi kubwa ya watumishi kushiriki mashindano hayo.
Michuano hiyo inatarajiwa kuwa pia fursa kwa watumishi kutoka Jiji la Arusha kushirikiana, kujenga afya na kuimarisha mshikamano kupitia michezo, huku wakibeba dhamana ya kulitangaza Jiji la Arusha katika medani ya kitaifa.
