Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba leo Agosti 15, 2026 ameendelea kutatua kwa njia ya maridhiano migogoro sugu inayowakabili wananchi na mara hii ametatua mgogoro wa ardhi kati ya Bi. Alia Shariff na Bi Devotha Delfina Elisei uliodumu miaka 28 katika eneo la Goba jijini Dar es salaam .

Bi. Alia Shariff, mkazi wa Dar es Salaam, alimwandikia barua Mheshimiwa Waziri Mkuu tarehe 20 Januari 2026, akiomba amsaidie kutatua mgogoro huo na katika barua hiyo, alieleza kuwa eneo analolalamikia limemilikiwa na wanae tangu mwaka 1998 na kwa muda wote huo ametafuta suluhu ya jambo hilo bila mafanikio. 

Waziri Mkuu alituma Timu ya Watalaam kutoka Ofisini kwake ikiongozwa na Mwenyekiti ambaye pia ni Msaidizi wa Waziri Mkuu – Mahusiano, Asasi za Kiraia na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Bw. Tryphone Mkolokoti, na Katibu wake ambaye pia ni Msaidizi wa Waziri Mkuu – Masuala ya Ardhi, Bw. Senso Magessa ambayo ilishirikiana na Kamishina Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es salaam, Shukuruni Kyando, Watalaam wa Ardhi Manispaa ya Kinondoni pamoja wa viongozi wa Kata na Mtaa wa Goba lilipo eneo lenye mgogoro.

Timu iliitisha vikao vya usuluhishi na kutembelea eneo la mgogoro vilivyowahusisha Watalaam wa masuala ya ardhi Mkoa wa Dar es salaam na wilaya ya Kinondoni, majirani na wazee walioishi miaka mingi pamoja na wapima ardhi ambao walihakiki na kubainisha mipaka halali ya viwanja Namba 202, 203, 204 na 205, vilivyopo Goba, jijini Dar es Salaam vilivyokuwa na mgogoro.

Baada ya uchambuzi wa nyaraka, maelezo ya pande mbili zilizohuka katika mgogoro huo na upimaji uliofanywa imebainika kuwa uamuzi wa Mahakama umeelekeza kuwa kiwanja Na. 202 chenye ukubwa wa zaidi ya mita za mraba 3,000 ambapo Devota anamiliki mita za mraba 1,000 ndicho kiini cha mgogoro.

Pande zote mbili zimekubaliana kuheshimu hukumu, amri na maamuzi halali ya Mahakama, pamoja na kufuata taratibu zinazotakiwa na mamlaka za ardhi katika kubainisha na kutekeleza haki za kila upande na kuepuka vitendo vinavyoweza kuibua mgogoro tena.

Nayo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam imeelekezwa kusimamia na kuhakikisha Ofisi ya Ardhi ya Wilaya ya Kinondoni inakamilisha haraka taratibu za kitaalamu za kugawa kiwanja Na. 202 ambacho ni kiini cha mgogoro kwa mujibu wa maamuzi ya Mahakama na makubaliano yaliyofikiwa katika maridhiano hayo.

Utiaji saini nyaraka za maridhiano hayo ulifanyika kwenye eneo lililokuwa na mgogoro

 Goba jijini dar es salaam na kushuhudiwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa wa Dar es salaam, Shukuruni Kyando, Watalaam wa Ardhi Manispaa ya Kinondoni na Mkoa wa Dar es salaam, Watalaamu kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, Viongozi wa eneo la Goba na wananchi.

Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dar es salam Shukuruni Kyando alitumia fursa hiyo kutoa elimu ya namna sahihi na ya haraka ya kubatilisha hati miliki ya ardhi na kupata hati mpya na halali katika maeneo yenye migogoro ambayo utatuzi wake ulisababisha kiwanja hicho kugawanywa kwa mmiliki zaidi ya mmoja.  

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amedhamiria kutatua baadhi ya migogoro inayowakabili wananchi kwa maridhiano yanayoendeshwa na Timu yake ya Watalaam aliyoiagiza kufanya kazi hiyo kwa kuzingatia maamuzi ya vyombo vya sheria, taratibu, kanuni na utu. Hatua hiyo imewafanya wananchi wengi kumwandikia barua za malalamiko yao na kujitokeza kwa wingi kutoa kero zao katika mikutano anayoihutubia.