Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mwalimu Fakii Raphael Lulandala ameongoza mamia ya wakazi wa eneo hilo kwenye mazoezi ya mbio fupi za kujiandaa na Manyara Tanzanite Marathon zinazotarajiwa kufanyika mjini Babati Agosti 22, 2026.
Mwalimu Lulandala akizungumza na wakazi wa mji mdogo wa Mirerani, watumishi wa Halmashauri, wakuu wa vitengo, idara na mashirika amewashukuru kwa kujitokeza kushiriki mbio hizo.
“Lengo la mbio fupi za leo ni kujiandaa na kuhamasisha kujiandikisha na kujitokeza kwa wingi kwenye Manyara Tanzanite Marathon itakayofanyika mjini Babati,” amesema Mwalimu Lulandala.
Amewaasa watu wa Wilaya hiyo ambao hawajajiandikisha wafanye hivyo kupitia mbio za kilomita tano, 10, 21, na 42 pamoja na kilomita mbili za vijana na watoto.
Amesema lengo la mbio hizo ni kuchangia fedha za ujenzi wa wodi na kununua vifaa tiba vya watoto wachanga waliozaliwa kabla ya muda wao wa miezi tisa.
Amesema awali wodi hiyo itajengwa kwenye wilaya ya Hanang’ na vifaa tiba vitajengwa katika Wilaya nyingine kupitia fedha zitakazopatikana kwenye mbio hizo.
Amesema mbio hizo zimeshasajiliwa hivyo zitakuwa zinafanyika kila mwaka kwa lengo la kutafuta fedha za kuboresha huduma ya afya kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa wa Manyara.
“Nawashukuru wote walioshiriki katika mbio fupi hizi za kujiandaa na Manyara Tanzanite marathon ambayo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Mwigilu Lameck Nchemba,” amesema DC Lulandala.
Afisa mtendaji Mkuu wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani (TEO) Isack Mgaya amesema makundi mbalimbali yameshiriki mbio fupi hizo na hamasa imekuwa kubwa mno.
“Watumishi wote wa mji mdogo wa Mirerani wameshajiandikisha kushiriki mbio za Manyara Tanzanite Marathon itakayofanyika mjini Babati,” amesema Mgaya.
Kocha wa umoja wa wakimbiaji Mirerani, Issa Katuga amesema wanachama wake wameshajiandaa na sare maalum ya kushiriki Manyara Tanzanite Marathon.
Mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite, Lawrencia Charles amesema wamejipanga kikamilifu kushiriki Manyara Tanzanite Marathon itakayofanyika mjini Babati.
Amesema wafanya biashara wa madini ya Tanzanite wamejiandikisha kwa wingi na wanajiandaa na mazoezi kwa lengo la kushiriki mbio hizo.
