Jamhuri ya Afrika Kusini imeipongeza Tanzania kwa mchango na juhudi zake katika kupunguza tatizo la njaa na kuimarisha usalama wa chakula katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Ronald Lamola, wakati akiwasilisha hotuba ya kufunga Mkutano wa Baraza la Mawaziri la SADC uliofanyika tarehe 12 hadi 14 Agosti 2026 jijini Durban, Afrika Kusini.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya (Mb.), kubainisha kuwa uzalishaji wa chakula nchini umeongezeka kutoka tani milioni 22.80 mwaka 2024/2025 hadi tani milioni 23.80 mwaka 2025/2026, sawa na ongezeko la asilimia 4.3.
Akizungumzia mafanikio hayo, Mhe. Millya alisema uwiano wa taifa wa kujitosheleza kwa chakula umefikia asilimia 130, hali inayoonesha kuwa uzalishaji wa ndani unatosheleza mahitaji ya chakula nchini na kuwezesha kuwepo kwa ziada inayoweza kusaidia nchi nyingine wanachama wa SADC.
Mbali na Tanzania, Mhe. Lamola pia alizipongeza Jamhuri ya Zambia, Zimbabwe na Namibia kwa hatua kubwa walizopiga katika kupunguza tatizo la njaa na kuimarisha usalama wa chakula.
Hata hivyo, alisema pamoja na hatua zilizopigwa na nchi hizo, bado watu milioni 58 katika ukanda wa SADC wanaishi katika hali ya kutokuwa na uhakika wa kupata mlo wao siku, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuongeza kasi ya juhudi za kukabiliana na uhaba wa chakula.
Mhe. Lamola, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la SADC kwa kipindi cha Agosti 2026 hadi Agosti 2027, amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuongeza kasi ya utekelezaji wa mikakati ya pamoja ya kukabiliana na uhaba wa chakula, pamoja na kuimarisha uzalishaji wa kilimo na biashara ya mazao ya chakula ndani ya ukanda huo.
