DAR ES SALAAM. 

Serikali imeweka mkakati wa kupunguza muda ambao meli za mafuta hutumia bandarini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza ufanisi katika upokeaji, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za mafuta nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, anayeshughulikia Mafuta na Gesi Dkt. James Mataragio, amesema hayo wakati wa ziara ya kukagua miundombinu ya mafuta katika eneo la Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Tanzania International Petroleum Reserves Limited (TIPER), Leo Augosti 14,2026 Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mataragio amesema Serikali inalenga kuhakikisha meli zinazowasili nchini zinapata huduma kwa wakati, zinashusha mafuta kwa ufanisi na kuondoka bandarini bila ucheleweshaji usio wa lazima.

“Ni matarajio ya Serikali kuona meli zikifika, zinashusha mafuta na kuondoka. Kila taasisi inapaswa kufahamu jukumu lake na kujipanga ipasavyo,” amesema.

Ameeleza kuwa moja ya changamoto zinazochangia meli kukaa bandarini kwa muda mrefu ni kasi ndogo ya upokeaji na uondoshwaji wa mafuta katika baadhi ya maghala binafsi. Hali hiyo husababisha meli kusubiri na kuongeza msongamano bandarini.

Kutokana na changamoto hiyo, Dkt. Mataragio ameutaka Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kuimarisha usimamizi wa wamiliki wa maghala binafsi na kuhakikisha wanaweka miundombinu inayokidhi mahitaji ya uendeshaji.

Amesema wamiliki wa maghala wanapaswa kuboresha pampu na vifaa vingine vinavyotumika kupokea mafuta, hasa vinapokuwa vimechakaa au havina uwezo unaohitajika.

Kwa mujibu wa Dkt. Mataragio, ucheleweshaji wa meli bandarini huongeza gharama za uendeshaji, zikiwemo gharama za meli kusubiri, ambazo hatimaye zinaweza kuathiri bei ya mafuta kwa mwananchi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa PBPA, Bw. Erasto Simon, amesema taasisi hiyo itakutana na wadau muhimu katika sekta ya mafuta, wakiwemo kampuni za uuzaji wa mafuta (OMCs) na TPA, kwa ajili ya kupitia na kuboresha Mwongozo wa Taratibu za Uendeshaji (Standard Operating Procedure Manual).

Amesema mapitio hayo yanalenga kuweka wazi majukumu, muda wa utekelezaji na uwajibikaji wa kila mdau katika mchakato wa upokeaji na uhamishaji wa mafuta.

Hatua hiyo inatarajiwa kuimarisha uratibu kati ya meli na maghala ya kupokea mafuta, kupunguza muda wa meli kukaa bandarini na kudhibiti gharama zinazotokana na ucheleweshaji.

Katika ziara hiyo, Dkt. Mataragio aliambatana na Kamishna wa Mafuta kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Goodluck Shirima; Mtendaji Mkuu wa PBPA, Bw. Erasto Simon; Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed Gallus Abed; pamoja, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Mashariki, Mhandisi Lorivii Long’idu na wataalam kutoka Wizara ya Nishati.