Mbunge wa Jimbo la Mtumba Mh. Anthony Mavunde jana ameshiriki pamoja na wazazi,walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Gen. Musuguri iliyopo kata ya Ihumwa kuanzisha ujenzi wa uzio wa shule hiyo ikiwa ni sehemu wa utekelezaji wa ahadi alizozitoa mwaka jana wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Akizungumza shuleni hapo,Mbunge Mavunde amesema Shule hiyo inapakana barabara kuu iendayo Dar es salaam ambayo yanapita magari mengi na hivyo kuhatarisha usalama wa wanafunzi na pia kushindwa kufuatili vizuri masomo wakati wa vipindi vy kawaida.

“Tunaishukuru serikali chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa upanuzi wa barabara ambayo sasa itakuwa ni ya njia nne.

Hivyo ni muhimu kuanza mapema ujenzi wa uzio huu ili kulinda usalama wa watoto wetu kwa kuwa na eneo moja tu la geti la mbele la watoto kupita kuliko ilipo hivi sasa ambapo watoto huvuka kupitia eneo lililopakana na barabara.

Lakini pia sasa watapata utulivu wa masomo kwa kutenganisha shughuli za barabarani na mazingira ya hapa shuleni”Alisema Mavunde

Katika kuanzisha ujenzi huo,Mbunge Mavunde amechangia Matofali 5000 na mifuko ya saruji 250 kuunga mkono juhudi hizo za wananchi.

Naye Diwani wa Kata ya Ihumwa,Mh. Edward Magawa amesema hatua ya ujenzi wa uzio wa shule hiyo kongwe itasaidia kubadilisha muonekano wa shule hiyo na kuwapa utulivu wa kimasomo wanafunzi muda wote.