Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akisikiliza maelezo ya Mradi wa Makaazi wa Amani Residency kutoka kwa Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Mhe. Shariff Ali Shariff, wakati wa uzinduzi wa mradi huo Kizimkazi, Kusini Unguja, Agosti 13, 2026.

……………

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa Sekta Binafsi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa makaazi bora na miradi mingine ya uwekezaji inayochochea ukuaji wa uchumi na kufungua fursa za ajira kwa wananchi.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 13 Agosti 2026, alipozindua na kukagua Mradi wa Makaazi wa Amani Residency, uliopo Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, ikiwa ni sehemu ya matukio ya Tamasha la Kizimkazi 2026.

Rais Dkt. Mwinyi amempongeza mwekezaji wa Bopar Enterprises Ltd, Bw. Said Bopar, kwa kuwekeza katika Mradi wa Amani Residency, pamoja na Mohammedi Builders Ltd kwa kazi nzuri ya ujenzi wa mradi huo.

Amesema uwekezaji huo unaonesha umuhimu wa ushiriki wa Sekta Binafsi katika kuongeza upatikanaji wa makaazi bora, kufungua fursa za ajira na biashara, pamoja na kuongeza shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.

Dkt. Mwinyi amesema Tamasha la Kizimkazi limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo Kizimkazi na Mkoa wa Kusini Unguja kwa ujumla, hususan katika makaazi, majengo ya biashara, hoteli na sekta nyingine za maendeleo.

Amesema Serikali itaendelea kuhimiza viongozi katika ngazi mbalimbali kutangaza fursa zilizopo katika maeneo yao na kushirikiana kwa karibu na Sekta Binafsi ili uwekezaji unaofanyika uweze kuleta manufaa kwa wananchi, wawekezaji na Serikali.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali, kupitia Shirika la Nyumba Zanzibar, inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya makaazi, sambamba na kuhamasisha ushiriki wa Sekta Binafsi na taasisi za fedha katika kuongeza upatikanaji wa nyumba bora na salama.

Ameeleza kuwa maendeleo ya makaazi yanaendelea kwenda sambamba na juhudi za Serikali za kuimarisha miundombinu ya msingi, ikiwemo barabara, maji, umeme na mifumo ya mawasiliano, ili kukidhi mahitaji ya wananchi na uwekezaji unaoendelea kuongezeka.

Amesema Mradi wa Amani Residency utaongeza pia uwezo wa Kizimkazi kupokea wageni na kutoa huduma za makaazi ya kisasa, jambo litakalochangia kuimarisha shughuli za utalii na kuongeza mvuto katika Mkoa wa Kusini, Unguja.

Naye, Bw. Said Bopar mmiliki wa mradi wa nyumba za Amani Residency amesema utekelezaji wa mradi huo umeungwa mkono na Benki ya CRDB, kupitia mkopo unaofikia asilimia 70 ya gharama za mradi, akieleza kuwa ushirikiano wa taasisi za fedha una nafasi muhimu katika kuwezesha uwekezaji mkubwa wa Sekta Binafsi.

Akitoa maelezo kuhusu mradi huo, Mwakilishi wa Mohammedi Builders Ltd, Mhandisi Taher Mustafa Jafferji, amesema Amani Residency imejengwa katika eneo la ekari 11, ikiwa na jumla ya nyumba 82 za makaazi zinazojumuisha villa 18 na apartment 64, pamoja na migahawa, maduka, supermarket, ukumbi wa mazoezi, sauna, bwawa la kuogelea na maeneo ya mapumziko, michezo na burudani.