Na Meleka Kulwa — Fullshangwe Blog, Dodoma
Mkurugenzi Mtendaji wa TAWLA na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake la Stand for Her Land, Wakili Tike Mwambipile, amesema mila na desturi zimekuwa miongoni mwa changamoto zinazowafanya wanawake kushindwa kumiliki ardhi, licha ya mabadiliko makubwa yaliyopo katika jamii.
Ameyasema hayo Agosti 13, 2026, katika siku ya pili ya Kongamano la Haki za Ardhi za Wanawake lililofanyika jijini Dodoma kuanzia Agosti 12 hadi 13, 2026.
Amesema wanawake wa sasa wamesoma, wanafanya kazi na wanashiriki katika shughuli za kiuchumi, hivyo ni muhimu kujenga mazingira yatakayowawezesha wanawake na wanaume kuwa na haki sawa katika umiliki wa mali.
Amesema kampeni ya “Linda Ardhi ya Mwanamke” hailengi kumchukulia mwanaume nafasi yake, bali kuhamasisha umiliki wa pamoja na kuhakikisha wanawake wanapata fursa ya kujikwamua kiuchumi.
Aidhaz amebainisha Kuwa ukosefu wa umiliki wa ardhi na hali duni ya kiuchumi imekuwa ikiwafanya wanawake wengi kuwa katika mazingira magumu, ikiwemo kukosa sehemu ya kwenda wanapokabiliwa na changamoto za kifamilia na ukatili wa kijinsia.
Amesema changamoto ya fedha na mila na desturi bado ni kubwa katika utekelezaji wa kampeni hiyo, lakini juhudi zinaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
“Tunajivunia kuna maeneo mengine ambayo tulifikiria tutaweza kuyafikia, sasa hivi tunayafikia kama kule Meru kwa wale mashiri, wale viongozi, kule Manyara,” amesema.
Amesema ushirikishwaji wa viongozi wa kimila umeanza kuleta matokeo chanya katika baadhi ya maeneo, huku akibainisha kuwa bado changamoto ya uchumi inawafanya wanawake wengi kushindwa kununua ardhi hata pale ambapo mila na desturi zinaruhusu.
Kwa upande wake, mjasiriamali Olupa Sekajingo kutoka Kilimanjaro amesema mafunzo aliyoyapata kutoka Shirika la PELUM Tanzania pamoja na TGNP yalimwezesha kuanza kutumia mbegu za asili katika kilimo ekolojia.
Amesema awali alikuwa akilima mahindi ya hybrid, lakini baada ya kupata mbegu za asili alianza kuzitumia katika mashamba yake na mwaka 2025 zilionesha matokeo mazuri.
Akibainisha Kuwa amelima gunzi jekundu linaloitwa “Kaptula” kwa jina la Kipare, ikunguru pamoja na mahindi mekundu.
“Mahindi haya yanazaa vizuri sana. Yanastahimili ukame, yanavumilia maradhi, na pia yana afya kwa mlaji,” amesema.
Aidha, amewataka wanawake kulima mbegu za asili akisema zinastahimili ukame na zinaweza kusaidia katika kipindi cha mabadiliko ya tabianchi.
Amesema matumizi ya kilimo ekolojia pamoja na mbegu za asili yameendelea kumpa matokeo mazuri katika shughuli zake za kilimo.



