Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba (Mb.), ametembelea mabanda ya Wizara ya Nishati na taasisi zake katika Maonesho ya Tamasha la Kizimkazi yanayoendelea Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

Akiwa katika mabanda hayo, Mhe. Salome amezungumza na wataalam pamoja na kujionea namna wanavyotoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali katika Sekta ya Nishati.

Mhe. Salome amewapongeza watendaji wa Wizara na taasisi zake kwa kutumia maonesho hayo kuwaelimisha wananchi kuhusu juhudi zinazofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha Sekta ya Nishati na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati katika Sekta ya Nishati, ambapo baadhi ya miradi imekamilika ukiwemo mradi wa Julius Nyerere wa megawati 2,115 na mradi wa umeme jua Kishapu ambao awamu yake ya kwanza imekamilika na kuzalisha megawati 50.

Amesema kuwa miradi mingine inaendelea kutekelezwa, ikiwemo Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), pamoja na miradi ya umeme, gesi asilia na nishati safi ya kupikia.

Katika nishati safi ya kupikia amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wanachi ili kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo huku ikiendelea kusambaza teknolojia na miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwa taasisi na wananchi.

Katika maonesho hayo amewataka wataalam kuendelea kutoa elimu ili wananchi wafahamu hatua zinazopigwa na Serikali katika Sekta ya Nishati, manufaa ya miradi inayotekelezwa pamoja na fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.

Wizara ya Nishati na taasisi zake zinashiriki Maonesho ya Tamasha la Kizimkazi yanayofanyika Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, kuanzia Agosti 12 hadi 14, 2026.