Na Meleka Kulwa — Fullshangwe Blog, Dodoma
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amesema ardhi si tu rasilimali ya kiuchumi, bali ni msingi wa maisha, maendeleo, usalama wa familia na ustawi wa jamii, hivyo ni muhimu kujenga jamii yenye usawa kwa wanawake kupata nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya jamii kwa maendeleo endelevu.
Ameyasema hayo Agosti 12, 2026, alipomwakilisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, katika ufunguzi wa Kongamano la Haki za Ardhi za Wanawake linalofanyika jijini Dodoma kuanzia Agosti 12 hadi 13, 2026.
Aidha, Amebainisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuweka mazingira ya kisera na kisheria yanayolinda na kukuza haki za wanawake katika kupata, kumiliki, kutumia na kunufaika na ardhi, sambamba na kushiriki katika ngazi za maamuzi yanayohusu ardhi.
Ameongeza kuwa Sera ya Ardhi imeweka wazi haki na fursa sawa kwa wanawake na wanaume katika kupata haki za ardhi, huku sheria kuu mbili za ardhi, ikiwemo Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Sura ya 114, zikiweka msingi wa usawa wa kijinsia kwa kutambua haki ya kila mwanamke kupata, kumiliki, kutumia na kufanya miamala ya ardhi kwa kiwango na masharti sawa na mwanaume.
Amesema sheria inapoweka utaratibu huo, mila na desturi zinapaswa kuendana na sheria, kwa kuwa Tanzania inaongozwa kwa Katiba, sheria na utaratibu.
“Kwa hiyo kama unazungumzia babu zetu, mila zetu haziruhusu, huu sio muda wake,” amesema Mmuya
Aidha, Mhe. Mmuya amesema taarifa za Serikali zinaonesha kuwa asilimia 38 ya wanawake nchini Tanzania wanamiliki ardhi, akibainisha kuwa hiyo ni asilimia kubwa ikilinganishwa na changamoto zilizokuwepo hapo awali.
Ameongeza kuwa mijini, maombi mengi ya hati na uhamisho wa hati yanafanywa na wanawake, huku akisisitiza kuwa vijijini bado kuna umuhimu wa wanawake wengi zaidi kumiliki ardhi kwa kuwa shughuli nyingi za kiuchumi zinazogusa watu wengi, ikiwemo kilimo na ufugaji, zinafanyika kwenye ardhi ya vijiji.
Katika eneo la utatuzi wa migogoro, Mhe. Mmuya amesema Serikali pia imeweka msingi wa ushiriki wa wanawake kupitia Sheria ya Mahakama za Migogoro ya Ardhi, Sura ya 216, ambayo imeweka utaratibu wa kuhakikisha wanawake wanawakilishwa katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya kupitia nafasi za ushauri.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TAWLA, Tike Mwambipile, amesema ushirikiano wa wadau mbalimbali ni muhimu katika kulinda haki za wanawake katika umiliki wa ardhi, akibainisha kuwa wameona matokeo makubwa kutokana na uwepo wa sheria ya ardhi inayoweka wazi kuwa mwanamke na mwanaume wana haki katika umiliki wa ardhi.
Ameongeza kuwa wanawake wengi wameendelea kumiliki ardhi kutokana na kuwepo kwa sheria hiyo, huku akisisitiza kuwa ardhi si udongo pekee, bali ni utu, heshima na uhai wa familia.
Amesema bado kuna changamoto ambapo mwanamke anayefanya shughuli za kilimo na kutumia nguvu zake kulisha familia na taifa anaweza kukumbwa na migogoro ya kifamilia au kufiwa na mwenza, kisha kuambiwa hana haki ya kuendelea kumiliki ardhi na kutakiwa kuondoka.
Amebainisha kuwa hali hiyo ni dhuluma inayohitaji ushirikiano wa wadau kuishughulikia, akisema TAWLA imeanzisha kampeni kwa kushirikisha wadau mbalimbali, wakiwemo Wizara ya Ardhi na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, katika juhudi za kulinda haki za wanawake katika umiliki wa ardhi.
Naye Mwenyekiti wa Landesa amesema kampeni nchini Tanzania imejikita katika maeneo manne, ikiwemo kukabiliana na mila na desturi kandamizi zinazomzuia mwanamke kumiliki ardhi, kumwezesha kiuchumi, kuhakikisha anashiriki katika vyombo vya maamuzi na kulinda haki zake katika uwekezaji mkubwa unaoendelea nchini.
Amesema umiliki salama wa ardhi kwa mwanamke una mchango mkubwa katika usalama wa chakula, kipato, lishe na elimu ya familia, huku pia ukisaidia kupunguza ukatili wa kijinsia na kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi na vyombo vya utawala.
Kongamano hilo la Kampeni ya “Linda Ardhi ya Mwanamke” limewakutanisha viongozi wa Serikali, wataalamu wa ardhi, wadau wa maendeleo na viongozi wa wanawake, likiwa na kauli mbiu isemayo “Imarisha Haki na Milki Salama za Ardhi na Hatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi kupitia Uongozi wa Wanawake wa Ngazi ya Jamii.”

