Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Mhe. Patrick Mwalunenge, wakati alipotembelea Ofisi za Mkoa za Chama cha Mapinduzi (CCM), jijini Mbeya, wakati wa ziara yake Mkoani humo.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza wakati wa Kikao chake na wajumbe wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya (hawapo pichani), wakati alipotembelea Ofisi za Mkoa za Chama cha Mapinduzi (CCM), jijini Mbeya, wakati wa ziara yake Mkoani humo.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb)(Watatu kulia), Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa (kulia), Mbunge wa Mbeya Mjini, Mhe. Patrick Mwalunenge (wa tatu kushoto), Mbunge wa Jimbo la Lupa-Chunya, Mhe. Masache Kasaka (wa pili kulia), Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela (wa pili) na wajumbe wengine wa CCM mkoa wa Mbeya, wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya Waziri wa Fedha kutembelea Ofisi za Mkoa za Chama cha Mapinduzi (CCM), jijini Mbeya, wakati wa ziara yake Mkoani humo. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Mbeya)

…………
Na. Joseph Mahumi, WF, Mbeya
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema Mkoa wa Mbeya na maeneo ya Nyanda za Juu Kusini yana fursa kubwa ya kuongeza mchango wake katika uchumi wa Tanzania kwa kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao na kukuza shughuli za viwanda.
Mhe. Balozi Omar amesema hayo alipokuwa akizungumza wakati alipotembelea Ofisi za Mkoa za Chama cha Mapinduzi (CCM), jijini Mbeya, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja mkoani humo.Alieleza kuwa eneo la Nyanda za Juu Kusini linachukua takribani asilimia 20 ya eneo lote la Tanzania, lakini mchango wake katika pato la Taifa bado haujaendana kikamilifu na ukubwa wa eneo na fursa zilizopo.

Mhe. Balozi Omar alisema hali hiyo inaonesha  kuwa bado kuna nafasi kubwa ya kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, madini, viwanda na sekta nyingine za uzalishaji ili Mkoa wa Mbeya na Nyanda za Juu Kusini kwa ujumla uwe na mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa Taifa.

“Bado tuna fursa kubwa sana ya kuimarisha mchango wetu katika pato la Taifa uendane na eneo tulilonalo, na si kwa sababu hatuna fursa,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aidha, katika kusisitiza uchakataji wa mazao, alisema kuwa Serikali itaendela kuweka mkazo mkubwa katika kuongeza thamani ya mazao ndani ya nchi ili nchi iondokane na mfumo wa kuzalisha mazao na kuyauza bila kuyachakata, hatua ambayo itasaidia kuongeza ajira, mapato kwa wananchi na mapato ya Serikali, huku ikiiwezesha Tanzania kunufaika zaidi na mnyororo mzima wa thamani wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

“Msisitizo wetu uwe kwenye mnyororo wa thamani, Tunaweza kulima, kuvuna na kuuza mazao, lakini tunahitaji kuwa sehemu kubwa zaidi ya mnyororo wa thamani kwa kuhakikisha uchakataji unafanyika hapa nchini,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Alisema badala ya Tanzania kubaki katika hatua za awali za uzalishaji na kuuza malighafi, ni muhimu kuongeza uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao ili bidhaa zinazotokana na rasilimali za Tanzania ziweze kuzalishwa nchini na kuuzwa katika masoko ya ndani na nje na hatua hiyo itasaidia kuongeza ajira, mapato ya wananchi na Serikali, pamoja na kuchochea ukuaji wa viwanda na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Akizungumzia shughuli za uchimbaji wa madini mkoani Mbeya, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi wa mazingira na afya za wachimbaji pamoja na wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka shughuli za uchimbaji, kwa kuwa pamoja na manufaa ya kiuchumi yanayotokana na uchimbaji wa madini, Serikali inapaswa kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa kuzingatia usalama wa afya za watu na mazingira.

Kuhusu changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika Wilayani Chunya, Mhe. Balozi Omar alisema kuwa Serikali itafanya jitihada ya kuboresha miundombinu ya umeme utakaowezesha uchimbaji na uzalishaji wa dhahabu ufanyike kwa ufanisi na kuongeza tija kwa wananchi na mapato ya Serikali kwa ujumla.

Kwa upande wake Mbunge wa Mbeya Mjini, Mhe. Patrick Mwalunenge, alisema Mkoa huo una uwezo mkubwa wa kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa kupitia sekta za uzalishaji, hususan kilimo, viwanda na biashara.

Mhe. Mwalunenge alisema kuwa Mbeya inaendelea kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya uzalishaji wa mazao ya biashara kama chai, kahawa na kakao, hivyo kuna umuhimu wa kuweka mazingira yatakayowezesha wakulima kupata masoko ya uhakika pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao hayo.

“Nasisitiza Serikali ione umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya biashara na viwanda, ikiwemo ujenzi wa bandari kavu na kongani za viwanda, ili kuifanya Mbeya kuwa kitovu cha biashara na uzalishaji kwa Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani, kwa kuwa nafasi ya kijiografia ya Mbeya, pamoja na uzalishaji mkubwa wa kilimo katika Nyanda za Juu Kusini, inatoa fursa ya kuunganisha uzalishaji, uchakataji na masoko ya ndani na nje ya nchi” aliongeza Mhe. Mwalunenge.

Naye Mbunge wa Jimbo la Lupa-Chunya, Mhe. Masache Kasaka, alisema utekelezaji wa miradi ya maendeleo na upatikanaji wa fedha kwa wakati ni muhimu katika kuongeza kasi ya shughuli za uzalishaji na kuimarisha uchumi wa Mkoa wa Mbeya.

Mhe. Kasaka alisema Chunya ina mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa kupitia uzalishaji wa dhahabu na tumbaku, huku akieleza kuwa wilaya hiyo inaongoza kwa uzalishaji wa dhahabu miongoni mwa wachimbaji wadogo nchini, ikizalisha wastani wa kilo 400 kwa mwezi ambapo kama Serikali itaboresha upatikanaji wa umeme katika maeneo ya uzalishaji kutasaidia kuongeza uzalishaji wa dhahabu na kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi.

“Chunya ina fursa kubwa katika uzalishaji wa tumbaku, ambapo licha ya kilimo hicho kufanyika katika eneo dogo ukilinganisha na mikoa mingine, wilaya yetu imeendelea kuwa miongoni mwa wazalishaji muhimu na kama kutaimarishwa kwa miundombinu ya umeme, maji na barabara, pamoja na kukamilishwa kwa miradi inayotekelezwa, kutasaidia wananchi kutumia kikamilifu fursa zilizopo katika sekta za uzalishaji” alisema Mhe. Kasaka.