Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema kuwa Wizara kupitia Balozi zake duniani imekuwa kiungo muhimu cha kufanikisha na kuchochea mafanikio ya Serikali katika sekta zote nchini, iwe kilimo, uchukuzi, biashara au nishati.
Waziri Kombo amesema hayo wakati wa kikao kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) na Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kilichofanyika chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Najma Murtaza Giga Katika Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma Agosti 11, 2026.
“Kwa ufupi balozi zetu zinahusika na kila chembe ya mafanikio yanayoonekana hapa nchini ikiwemo upatikanaji wa fedha za ujenzi wa miundombinu kama vile reli ya kisasa, ununuzi wa ndege, upatikanaji wa vibali vya safari za ATCL, makusanyo ya maduhuli kupitia utalii na mauzo ya visa kwa wageni na upatikanaji wa fursa za uchumi wa buluu”, alisema Waziri Kombo
Balozi Kombo aliendelea kueleza kuwa Wizara kupitia Balozi zake imetekeleza majukumu yake ya msingi kwa kuzingatia Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, Toleo la Mwaka 2024 na kufanikiwa kupata mafanikio makubwa kwa manufaa ya nchi.
Mafanikio hayo ni pamoja na kupanua wigo wa uwakilishi, kuongezeka kwa fursa za biashara na uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje, kuimarika kwa uhusiano wa uwili, upatikanaji wa misaada na mikopo yenye masharti nafuu pamoja na kukua kwa matumizi ya lugha ya Kiswahili duniani.
Kwa upande wao, wajumbe wa Kamati wameipongeza Wizara kwa kazi nzuri inayofanya katika kuimarisha diplomasia na kulinda maslahi ya Tanzania na kuitaka kuongeza juhudi ili diplomasia ya Tanzania iendelee kung’ara duniani.

