Wanafunzi 6,800 kutoka nchi tano za Afrika Jumuiya ya Mashariki Mashariki tayari wamewasili mkoani Morogoro kushiriki Mashindano ya Michezo ya Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari ya Jumuiya hiyo (FEASSA) 2026, yatakayoanza kuanzia rasimi Agosti 12 hadi 23 mwaka huu katika viwanja mbalimbali katika manispaa ya morogoro.

Mashindano hayo yanayofanyika kwa mara ya 23 kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na mara ya tano nchini Tanzania, yatawakutanisha wanafunzi kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro, Mkuu wa Mkoa huo, Adam Kighoma Malima, amesema kuwa serikali kupitia ofisi ya waziri mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa TAMISEMI Imejipanga kuhakikisha unakuwa mwenyeji bora wa mashindano hayo, huku jumla ya viwanja 21 na maeneo manane ya malazi yakitengwa kwa ajili ya washiriki.

Hata hivyo amewahakikishia washiriki wa mashindado kuwa ulinzi na usalama umeimarishwa vya kutosha na kuwataka wakazi wa Morogoro kuchangamkia fursa za biashara bila kusahau kuwakaribu wageni kujenga mahusiano bora kama ilivyo zoeleka kwa watanzania

Amesema Tanzania itawakilishwa na wanafunzi 1,510 kutoka mikoa 26, ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya ushiriki wa nchi hiyo katika historia ya mashindano hayo.

Kwa upande wa Morogoro, amesema mkoa utashiriki katika michezo 13 baada ya kufanya vizuri katika mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA yaliyofanyika mkoani Iringa Juni mwaka huu.

Kwa ujumla, FEASSA 2026 itakuwa na michezo 20 kwa shule za sekondari, sita kwa shule za msingi na minne kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Malima amesema ujio wa maelfu ya washiriki na wageni unatoa fursa kwa wananchi kunufaika kiuchumi kupitia biashara, usafiri, chakula, malazi na huduma mbalimbali, huku ukitoa nafasi ya kutangaza vivutio vya utalii vya Morogoro na Tanzania.

Ufunguzi rasmi wa mashindano hayo unatarajiwa kufanyika Agosti 16, ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Malima amewataka wananchi kujitokeza kushuhudia mashindano hayo na kuwakaribisha wageni kwa ukarimu, huku akivitaka vyombo vya habari kutumia fursa hiyo kuitangaza Morogoro na Tanzania kwa ujumla.