Eric Sosthenes – Meneja wa Biashara Mixx – Kanda ya Kaskazini
…………….
Arusha. Zaidi ya wakulima 2,000 wa kahawa, mbaazi na mazao mengine katika mikoa ya Arusha na Manyara wamenufaika na huduma za kifedha kidijitali za Mixx, zinazowawezesha kupokea malipo ya mazao, kupata mikopo na huduma za bima bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za kifedha.
Meneja wa Biashara wa Mixx by Yas Kanda ya Kaskazini, Eric Sosthenes, amesema matumizi ya huduma hizo yanawapa wakulima njia salama na rahisi zaidi ya kusimamia fedha zao, huku yakiwapunguzia muda na gharama zilizokuwa zikitumika kufuata huduma za kifedha.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane jijini Arusha, Sosthenes alisema kupitia huduma ya Mixx Kilimo, wakulima wanaweza kupokea malipo ya mazao moja kwa moja kwa njia ya kidijitali pamoja na kupata huduma nyingine za kifedha zinazolenga kusaidia shughuli zao za kilimo.
“Tunataka mkulima awe na uwezo wa kupokea fedha zake kwa usalama na kwa wakati bila kulazimika kusafiri umbali mrefu. Kupitia Mixx Kilimo, tunarahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha zinazomsaidia mkulima kuendesha shughuli zake na kujiendeleza,” alisema.
Alisema huduma hiyo ni sehemu ya jitihada za Mixx kuongeza ujumuishaji wa kifedha miongoni mwa wakulima, hasa wale waliopo maeneo ambayo upatikanaji wa huduma za kawaida za kifedha umekuwa ukihitaji muda na gharama zaidi.
Baadhi ya wakulima wanaotumia huduma hiyo, akiwemo Ezekiel Mlingi na Baraka Emmanuel, walisema matumizi ya huduma za kidijitali yamewapunguzia changamoto ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za kifedha.
Walisema uwezo wa kupokea na kufanya miamala kupitia simu umewarahisishia kusimamia fedha zao na kutumia muda zaidi katika shughuli za uzalishaji.
Mixx imesema itaendelea kutumia huduma ya Mixx Kilimo kuwafikia wakulima wengi zaidi na kuwawezesha kupata huduma za kifedha kwa njia salama na rahisi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutumia teknolojia kuboresha shughuli za kilimo na maisha ya wakulima.
