Na Munir Shemweta, Bariadi, Simiyu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amesema Wizara yake iko tayari kushirikiana na mikoa inayounda Kanda ya Ziwa Mashariki pamoja na Wizara ya Kilimo na wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuandaa ramani ya uwanja ikiwemo mpangilio kulingana na mahitaji ya eneo la Viwanja vya Maonesho Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu.
Mikoa inayounda kanda ya Ziwa Mashariki katika maonesho ya Wakulima (Nanenane) ni mkoa wa Simiyu, Mara Pamoja na Shinyanga.
Dkt. Akwilapo ameyasema hayo Agosti 8, 2026 wakati akifunga Maonesho na Sherehe za Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) Kanda ya Ziwa Mashariki, yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu.
Amesema, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pia itasaidia kutoa muongozo wa umiliki wa eneo la uwanja na kuandaa mpango endelevu wa matumizi yake.
Kwa mujibu wa Waziri huyo wa ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, upangaji mzuri wa eneo ni msingi muhimu katika kuhakikisha shughuli na miundombinu inayotekelezwa katika viwanja hivyo inakuwa ya kudumu, inatumika kwa ufanisi na inaepusha migongano ya matumizi ya ardhi hapo baadaye.
“Wizara yetu iko tayari kushirikiana na mikoa inayounda Kanda ya Ziwa Mashariki, Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kutayarisha ramani na mpangilio wa matumizi ya eneo hili kulingana na mahitaji yaliyopo na yajayo,” amesema Dkt. Akwilapo.
Akigeukia upande wa Maonesho ya Wakulima (Nane nane) katika kanda ya Ziwa Mashariki aliyoyafunga rasmi, Dkt Akwilapo ambaye alikuwa mgeni rasmi ametoa wito maonesho hayo kufanyika kuanzia ngazi za Vijiji, Kata, Mitaa na Halmashauri alizozieleza kuwa huko ndiko wananchi wanakoishi.
Kufanyika kwa maonesho kuanzia ngazi hizo itasaidia kuwawezesha waliokusudia kuona na kujifunza teknolojia mbalimbali katika maeneo yao huko waliko’’. Amesema.
Amezishauri mamlaka za serikali za mitaa kuratibu ili maonesho hayo yaweze kufanyika katika ngazi za vijiji, kata, mitaa na wilaya kwa lengo la kuleta mapinduzi katika kilimo, mifugo na uvuvi.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha amesema maonesho na sherehe za wakulima (Nane nane) katika mkoa wake yalilenga kutoa fursa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kujifunza, kubadilishana uzoefu, kujenga ushirikiano na kutangaza bidhaa wanazozalisha katika maeneo yao.
Amewashukuru washiriki wa maonesho hayo kwa kuonesha mbinu mbalimbali alizozieleza kuwa zimesaidia wananchi kujifunza teknolojia bora katika mnyonyoro wa thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Akwilapo alitembelea Banda la Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Simiyu ambapo alipata fursa ya kukabidhi hati miliki za ardhi kwa baadhi ya wananchi wa Bariadi mkoani Simiyu waliokamilisha taratibu za kumilikishwa maeneo yao.
Akizungumza baada ya kukabidhi hati hizo, Dkt. Akwilapo aliwataka wananchi waliopokea hati hizo kuhakikisha wanazingatia masharti yote yanayoambatana na umiliki wa ardhi zao.
Maonesho na Sherehe za Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) Kanda ya Ziwa Mashariki, yamefungwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo kwenye Viwanja vya Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu.

