Na OWM–TAMISEMI, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amemhakikishia Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa Ofisi yake itatekeleza kikamilifu jukumu la kuisimamia Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), kwa lengo la kuhakikisha sera na mipango ya Serikali ya kuboresha usafiri wa umma jijini Dar es Salaam inafanikiwa.
Prof. Shemdoe ametoa kauli hiyo leo, Agosti 7, 2026, jijini Dar es Salaam, alipotoa salamu za OWM–TAMISEMI kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mbele ya wananchi, mara baada ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua rasmi Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka, Awamu ya Pili (BRT II), unaohusisha barabara za Kilwa, Chang’ombe, Sokoine na Kawawa.
“Mheshimiwa Rais, kazi uliyotupa ya kuisimamia Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) tutaifanya kwa bidii, weledi na moyo wa uzalendo ili kufanikisha utekelezaji wa sera na mipango ya Serikali ya kuboresha usafiri wa umma,” amesema Prof. Shemdoe.
Akizungumzia mchango wa wadau katika kufanikisha mradi huo, Prof. Shemdoe amewashukuru wadau mbalimbali, wakiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), TANROADS, wakandarasi, washauri elekezi na watoa huduma, kwa ushirikiano wao uliowezesha kukamilika na kuzinduliwa kwa BRT II.
Amesema mradi huo unalenga kupunguza changamoto za usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam wanaotumia barabara za Kilwa, Chang’ombe, Sokoine na Kawawa, pamoja na kuboresha ufanisi wa usafiri wa umma jijini humo.
Akieleza faida za mabasi ya kisasa ya mwendokasi kwa wananchi na mazingira, Prof. Shemdoe amesema mabasi 60 yaliyoanza kutoa huduma katika njia ya Mbagala–Posta yamechangia kupunguza msongamano wa magari yanayoelekea katikati ya jiji, baada ya kuondoa daladala 400 kati ya daladala 1,627 zilizokuwa zikihudumia wakazi wa eneo hilo.
Amesema hatua hiyo si tu inaboresha usafiri kwa wananchi, bali pia inachangia kupunguza uzalishaji wa hewa yenye kiwango kikubwa cha gesi ya kaboni dioksidi (CO₂), inayozalishwa wakati injini za magari zinapochoma mafuta ya petroli na dizeli.
Kwa hatua hiyo, Serikali inaendelea kuimarisha usafiri wa umma wenye ufanisi na unaozingatia mahitaji ya wananchi, huku ikiweka mkazo katika kupunguza msongamano wa magari na athari za uzalishaji wa hewa ukaa jijini Dar es Salaam.

