* Wapo viongozi wa juu, wananchi na wanafunzi kwa ajili ya kujionea wanyamapori kutangaza utalii wa ndani

*Tembo Mary awa kivutio kwenye bustani ya wanyamapori kutokana na historia yake na uelewa wake wa hali ya juu

Na Neema Chalila Mbuja

WIZARA ya Maliasili na Utalii imevunja rekodi ya kupokea wageni zaidi ya 17,000 kwa siku kwenye Maonesho ya mwaka huu ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi maarufu lama NANE NANE yanayoendelea kitaifa kwenye Viwanja vya John Malecela, Nzuguni Jijini Dodoma.

Makundi makubwa ya wananchi, wanafunzi na wadau mbalimbali wa uhifadhi na wanyamapori wamefurika kwenye banda l Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kuona wanyama aina mbalimbali waliopo kwenye bustani ya wanyamapori kwa lengo la kutangaza utalii wa ndani. 

Idadi hiyo inafanya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kuvunja rekodi ya kutembelewa na wananchi wengi ambapo Bi. Amina Saleh mmoja wa wananchi waliotembelea bustani ya wanyama anasema wamefurahishwa sana na ujio wa wanyamapori hao kwani hajawahi kuwaona wanyama ana kwa ana zaidi ya kwenye picha.

Tembo Mary aliyekuwa kwenye bustani hiyo ya Maonesho ya wanyamapori amekuwa kivutio kwa wanafunzi wengi na wananchi kwa ujumla kutokana na historia yake na usikivu alionao ambapo mwanafunzi Collins Msemwa wa Kato Victoria Academy anasema kuwa ziara hiyo ya shule imehamasisha wanafunzi wengi kupenda wanyamapori na kujifunza kwa kina tabia za wanyamapori hao.

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambayo ndiyo msimamizi wa wanyamapori imefanikiwa kuleta wanyama Kama Tembo, Simba, Nyumbu, Pofu, Ngiri maarufu Kama Kasongoyeye, Duma, Chatu, ndege Karani, Mbuni, ndege Korongo (Crane) ambaye ni alama ya nchi ya Uganda, na ndege Mwali (White Perican bird) mbalimbali waliopo kwenye bustani ya NANE NANE.