▪️Fidia Shilingi bil 8.5 Imeshalipwa kwa Wananchi Waliopisha Mradi
Na Adelina Johnbosco – MAELEZO
Tatizo la uhaba wa maji katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Dodoma linaelekea kupata ufumbuzi wa kudumu kufuatia ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Farkwa utakaoanza kujengwa Oktoba mwaka huu.
Bwawa hilo litakalojengwa wilayani Chemba, kata ya Farkwa mkoani Dodoma litakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 128 kwa siku na kuhifadhi lita bilioni 390 na linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 22.
Bwawa hili litahudumia hasa wilaya za Chemba, Bahi, Chamwino na maeneo mengine ndani na maeneo ya karibu na mkoa wa Dodoma, lengo ni kutokomeza kabisa upungufu wa maji ndani ya mkoa huo.
Ujenzi wa bwawa la Farkwa utatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya Shilingi bilioni 163.43 hadi kukamilika kwake.
Aidha, jumla ya Shilingi bilioni 8.5 zimelipwa kama fidia kwa wananchi kutoka katika vijiji viwili vya Mombose na Bubutole waliopisha ujenzi.
“Tuliambiwa tunahamishwa na kulipwa, mwaka 2017 tathmini ilifanyika katika maeneo yetu, ila ukiwa bado hujapokea kitu mkononi unaona kama haiwezekani, lakini mwaka 2019 tukalipwa fidia zetu, tukaanza maisha mapya na yenye matumaini zaidi katika kijiji cha Sankwaleto kwenye makazi mapya” Bi. Rahma Petro, mkazi wa Farkwa
Hadi hapa, tayari inaonekana Dodoma yenye ukijani wakati wote, iwe mvua iwe jua, hakuna tena ukame katika mkoa huu pale mradi huu utakapokuwa umekamilika, yale yaliyokuwa yanasubiriwa kufanyika wakati wa kipindi cha mvua pekee yatafanyika pia kipindi cha kiangazi.
“Tumeajiandaa kwa vingi kwa kweli, kijamii na kiuchumi, tutalima kilimo cha umwagiliaji, tutafuga samaki na mengine mengi, ni furaha tupu. Hii ilikuwa ni hadithi ya muda mrefu ambayo tumezaliwa tukaikuta kutoka kwa wazee wetu, hakika leo inatimia” Bw. Suleiman Gawa, mkazi wa Farkwa
Akiwa katika eneo utakapotekelezwa mradi huo, hivi karibuni, Bw. David Manyama, Mhaidrojiolojia ambaye ni mtaalam wa maji chini ya ardhi kutoka Wizara ya Maji, amebainisha uwepo wa maji ya akiba kwa watumiaji kutokana na wingi wa lita za maji utaokaozalishwa na bwawa hilo.
“Mradi huu unaanza mwezi Oktoba, 2026, maandalizi yako tayari na baada ya kukamilika kwa mradi, si kwamba utaondoa kero ya maji tu bali hata kuchochea miradi mbali mbali ya kiuchumi kama vile kilimo cha umwagiliaji kisichosubiri msimu, ufugaji wa samaki na itakuwa ongezeko la maji katika hifadhi ya pori la akiba Swagaswaga Chemba, wanyama hifadhini watapata maji ya kunywa ya kutosha tofauti na hali ilivyo kwa sasa” Bw. David Manyama, Mhaidrojiolojia
Mradi huu mwisho wake ni kuleta maji, lakini suala la ajira wakati na baada ya mradi ni vitu vinavotegemewa pakubwa. Mwenyekiti wa kijiji chenye makazi mapya cha Sankwaleto, akaongea kuhusu wazawa kupata fursa mbalimbali kutokana na mradi huo.
“Kama kiongozi tumeshashirikishwa na kuhakikishiwa kwamba, sisi wazawa tutapewa kipaumbele katika fursa mbalimbali zinazotokana na huu mradi ikiwemo ajira wakati na baada ya ujenzi, hivyo nawasihi vijana na wakazi wenzangu wa hapa kuwa tayari, tusikubali kukaa kinyonge katika kuchangamkia fursa katika hizi” Bw. Khalifa Salum, mwenyekiti wa kijiji chenye makazi mapya Sankwaleto
Si nyumba na umiliki wa ardhi pekee kwenye maeneo ya makazi mapya waliohamia wananchi waliopisha mradi, bali shule na zahanati vimejengwa kwa ajili ya kuwahudumia.
“Kijiji cha Sankwaleto kimejengwa shule ya msingi na imeshaanza kazi, kuna nyumba za walimu na wanafunzi wote waliokuwa wakisoma kule kwenye vijiji vya zamani wako kwenye shule mpya wanaendelea na masomo, hakuna kilichosimama, pia zahanati inayowahudumia wananchi, kwa kweli tunashukuru sana” – Bi. Agnes Msote, Diwani wa kata ya Farkwa
Kukamilika kwa Bwawa la Farkwa kunatarajiwa kuimarisha usalama wa maji katika jiji la Dodoma na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi katika mkoa huo.
Juhudi hizo zinaendana na azma ya Serikali ya kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji nchini kwa kuzingatia usimamizi endelevu wa rasilimali za maji na upatikanaji wake maeneo yote hasa katika maeneo ya vijijini pamoja na kuhakikisha juhudi za kufikisha huduma za maji katika vijiji vyote nchini linatimia ili kumtua mwanamke ndoo kichwani.
